Jeshi la Polisi Mkoa wa Ilala linamshikilia mtu mmoja
anayedaiwa kuhusika na shambulio lililofanywa na wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM), ambalo lililotokea Msongola kijiji cha Kidole, Chanika na kusababisha
watu kujeruhiwa na wanawake kudhalilishwa.
Vurugu hizo zinadaiwa kufanywa na moja ya kundi la watia nia
Jimbo la Ukonga.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Mkoa wa Ilala, Lucas Mkondya
alisema, tukio hilo
lilitokea juzi alasiri wakati wafuasi wa kundi la mtia nia mmoja lilipovamia na
kuliteka gari lililokuwa limebeba wafuasi wa CCM.
Alisema walioshambuliwa walikuwa kwenye gari aina ya Noah
ambao walikuwa wanatoka kwenye mkutano na walipofika eneo hilo walikutana na gari aina ya Jeep ambalo
watu waliokuwamo ndani walifanya unyama huo.
Kamanda alisema baada ya shumbulio, watu wanane waliokuwa
kwenye Noah walitoa ripoti polisi zilizowezesha kukamatwa kwa mtu mmoja ambaye
jina lake wamelihifadhi .
“Tunaendelea kumhoji mtu huyu kwa kesi iliyofunguliwa ya
shambulio, kati ya waliofungua kesi wanawake ni wanne,” alisema.
Alisema jeshi la polisi linaendelea kufuatilia wengine
waliohusika kwenye vurugu hizo.
Chanzo cha habari cha kuaminika kilichofanikiwa kufika eneo
la tukio na kushuhudia waliofanyiwa unyama huo, baada ya watu hao kuliteka gari
hilo walilipeleka
kwenye vichaka na kuanza kuwavua nguo wanawake na kuwafanyia udhalilishaji huo.
Chanzo hicho kimesema kuwa, watu hao waliwajeruhi wanaume
sita ambao mmoja alitobolewa tumboni na kukimbizwa hospitali ya Temeke kwa
matibabu.
Chanzo kilieleza kuwa, waliotekwa walisema watekaji hao
walikuwa wanawahoji kwa nini wameamua kumsapoti mgombea wa jimbo la Ukonga
(jina tunalo).
