“Kwa jina la Mwenyezi Mungu (Allah), Mungu mpaji, na mwenye
rehema….
Kwa miaka takribani 40 ama ilikuwa zaidi sikumbuki.
Nachokumbuka ni kuwa nilifanya kila nilichoweza kuwapa watu wangu nyumba,
hospitali na shule. Na kila walipohisi njaa niliwapa chakula. Niliifanya
Benghazi kutoka jangwa kuwa ardhi nzuri ya kilimo.
Nilifanya kila nililoweza kuwafanya watu wangu waelewe maana
halisi ya demokrasia; ambapo watu wa tabaka la chini niliwapa madaraka.
Lakini hawakuridhika. Hata aliyekuwa na nyumba ya vyumba
kumi, nguo mpya, na fanicha nzuri, hakuridhika. Alihitaji zaidi.
Kwa jinsi walivyokuwa wabinafsi walihitaji zaidi. Hivyo
wakawaambia Marekani kuwa wanataka “demokrasia” na “uhuru”. Hawakujua kuwa
“demokrasia” waliyoitaka ilikua ni mfumo wa unyonyaji ambapo mbwa mwenye nguvu
zaidi huwala mbwa wadogo.
Walikua hawasikii wala hawaoni. Walitaka “demokrasia”.
Wakasahau kuwa hata Marekani hakukuwa na huduma za afya za bure, dawa bure,
elimu bure na chakula cha bure. (Huduma hizi za bure zilipatikana Libya tu).
Nchini Marekani mtu masikini/fukara hana cha bure. Labda awe
ombaomba au avuje jasho kuhemea.
Haikujalisha nilifanya kwa kiasi gani bado hawakuridhika.
Lakini wapo waliojua mimi ni mtoto wa Gamal Abdel Nasser ,
mwarabu pekee halisi na kiongozi wa kiislamu tuliyewahi kuwa nae tangu enzi za
Salah-al-Deen.
Wakati Nasser anapigania mfereji wa Suez
kwa watu wake nami nilikua naipigania Libya kwa watu wangu. Nilikua
najaribu kufuata nyayo zake ili kuwaweka watu wangu huru kutoka kwenye makucha
ya wakoloni wanaotuibia.
Lakini kwa sasa niko mateka katikati ya majeshi makubwa ya
dunia katika historia. Mwanangu mpendwa mwenye asili ya Afrika, Obama anataka
kuniua.
Ili achukue uhuru wetu, achukue haki yetu ya huduma za bure
za afya, huduma za bure za elimu, na chakula chetu; na kutuletea mfumo mpya wa
kimarekani wa kuiba uitwao “Ubepari”
Lakini wote katika dunia ya tatu tunajua maana yake. Maana
yake ni kuwa “washirika” wanatawala mataifa, wanatawala dunia, na watu
wanaishia kuteseka.
Kwa hiyo hakuna mbadala kwangu. Lazima niwe na msimamo. Na
kama Mungu atapenda nitakufa kwa mapenzi yake.
Mapenzi yake yaliyofanya nchi yetu kuwa na ardhi yenye
rutuba, chakula bora, na huduma bora za afya. Mapenzi ya Allah yaliyowezesha
tukawasaidia kaka na dada zetu waafrika na waarabu waliokuwa na shida.
Sipendi kufa; lakini kama nitakufa ili kuiokoa ardhi hii,
kuokoa watu wangu, na wengine ambao ni kama wanangu; acha nife.!
Acha sauti hii iwe agano langu kwa dunia kuwa nilisimama
kupinga uvamizi wa NATO. Nilisimama kishujaa kupinga usaliti wa nchi za
magharibi na nia mbaya za kikoloni. Na hapa nimesimama na ndugu zangu waafrika,
kaka na dada zangu waislamu kama ngao yangu ya
matumaini.
Wakati wengine walipokuwa wanajenga majumba ya kifahari,
mimi niliishi kwenye nyumba ya kawaida na kwenye mahema. Siwezi kusahau maisha
yangu ya utoto kule Sirte.
Sikutapanya rasilimali za nchi yangu kipumbavu. Na kama
alivyokua Salah-al-Deen, kiongozi wetu katika uislamu, nilichukua kidogo sana
kwa ajili yangu, na sehemu kubwa niliwapa wananchi.
Watu wa magharibi wameniita “kichaa”, “mwendawazimu” lakini
wanajua ukweli kuwa mimi si kichaa wala mwendawazimu; ila waache waendelee
kudanganya. Wanajua hii ardhi ni huru na haipo kwenye himaya ya kikoloni. Huu
ndio msimamo wangu na dira yangu na imekuwa wazi kwa watu wangu.
Nitapambana hadi pumzi yangu ya mwisho ili watu wangu wawe
huru. Mwenyezi Mungu atusaidie tubaki waaminifu na tuwe huru.
— Mu’uammar Qaddafi.
