Fahamu kinachosababisha maumivu ya kichwa, harara, kiungulia mara kwa mara

Inaweza kukushangaza kuwa baadhi ya vyakula maarufu na vinavyopendwa, mathalani matunda ya jamii ya machungwa, machenza, malimao, ndimu, na mabalungi, vinaweza kukusababishia hisia za kuumwa.

Vyakula vingine katika kundi hili ni pamoja na mvinyo mwekundu, jibini, achari, nyama ya nguruwe, mtindi, mayai na vyakula vinavyoandaliwa kutokana na viumbe wanaovuliwa baharini (sea food).

Vingine ni nyama zilizochakatuliwa kama soseji, nyama zilizokaushwa, viporo vya nyama, yogurt, matunda ya jamii ya zambarau, matunda yaliyokaushwa,  vyakula vilivyochachuliwa na  Spinachi.

Kundi hili linajumuisha pia nyanya ikiwa ni pamoja na ketchup, tomato sausi, rangi bandia za vyakula na kemikali za kuongeza muda wa matumizi kwenye chakula na viungo kama vile mdalasini, pilipili ya unga na karafuu.

Vingine ni vinywaji kama vile chai, pombe,  chocolate, cocoa, na jamii ya cola,siki (vinegar) na vyakula vyenye siki kama vile achari na ketchup.

Hisia hizi zinajidhihirisha kwa dalili kama vile maumivu ya kichwa, kuwashwa kwa ngozi, msongo, kiungulia kikali, kubanwa kwa njia ya hewa (nasal congestion), nakadhalika.

Kama mwili wako unapata hisia za kuumwa (mizio) baada ya kula aina fulani za vyakula, ikiwa ni pamoja na hivyo nilivyoorodheshwa hapo, inawezekana unakabiliwa na tatizo lisilojulikana sana, japokuwa linawakabili watu wengi.

Ni tatizo la mwili wako kushindwa kuhimili uwepo wa homoni ya histamine (Histamine intolerance). Histamine ni kemikali ya kiorganic ambayo moja ya viasili vyake ni nitrogen.

Histamine ni moja ya kemikali zinazozalishwa na mwili pale kinga za mwili zinapojibu shambulizi au mashambulizi ya kitisho chochote dhidi ya mwili. Histamine hufanya kazi hii kwa kusababisha vimishipa vidogo vya damu kupanuka ili kuwezesha chembechembe nyeupe za damu, pamoja na baadhi ya protini kupita kwa urahisi, kwenda kupambana na kitisho chochote ambacho kimeuvamia mwili.

Kemikali hii hufanya pia kazi ya kuratibu baadhi ya shughuli za kifiziolojia zinazoendelea katika njia ya chakula, hasa tumboni. Histamine inafanya pia kazi kama ‘neurotransmitter’ yaani kemikali inayopokea, kukuza na kusafirisha mawimbi ya umeme yaliyobeba taarifa maalumu kutoka katika seli zinazounda mishipa ya fahamu hadi katika seli nyingine katika mwili.

Kama hujawahi kuisikia dhana ya mwili kushindwa kuhimili homoni ya histamine, tatizo hili huwakabili watu wengi.

Kwa kawaida ni vigumu kulitambua tatizo hili la mwili kushindwa kuhimili homoni ya histamine. Kwanza kabisa tatizo hili linazaa dalili nyingi na mara nyingi dalili hizi hudhaniwa kuwa zimetokana na matatizo mengine kabisa ya kiafya.

Madaktari wengi na wataalamu wa lishe hawajawahi kuisikia dhana hii na hivyo basi huishia kutoa matibabu ambayo hayalengi kabisa kiini cha tatizo. Ukweli wa mambo ni kwamba tatizo hili ni la kawaida sana, japokuwa halieleweki vyema.

Tofauti ya mizio ya kawaida inayotokana na vyakula na mizio inayoletwa na mwili kushindwa kuhimili Histamine.

Tatizo la mwili kushindwa kuhimili histamine kwa kawaida husababishwa na upungufu katika moja ya mifumo; kati ya mifumo miwili ya vimeng’enya vinavyohusika na mchakato wa uvunjifu wa Histamine ndani ya mwili. Mfumo huu ni ule ujulikanao kama diamine oxidase. Mfumo wa pili hujulikana kama histamine N-methyl transferase (HMT).

Upungufu katika huu mfumo wa DAO, ambao hupatikana katika utando unaozingira njia ya chakula (intestinal mucosa), unatajwa kuwa ndicho chanzo kikuu cha mwili kushindwa kuhimili histamine.

Ni dhahiri kwamba kuna tofauti za kimaumbile baina ya mtu na mtu, kuhusiana na utendaji kazi wa mifumo hii ya vimeng’enya.

Hata hivyo, inaaminika kuwa iwapo yeyote katika mifumo hii utakumbwa na dosari itakayosababisha ufanye kazi kwa kiwango cha chini, basi kutakuwa na histamine ya ziada mwilini na hali hii itasababisha kujitokeza kwa dalili nyingi mwilini zinazoshabihiana na mizio.

Miongoni mwa dalili hizi ni pamoja na: kuwashwa, hususan kwenye ngozi, macho, masikio na pua (pruritus). Harara kwenye ngozi (urticaria).

Kuvimba kwa tishu (angioedama), hususan katika uso, kinywani na wakati mwingine kwenye koo –kitu ambacho kinamfanya mtu ajenge hisia kama vile anakabwa.

Matatizo mengine ni kushuka kwa shinikizo la damu (hypotension), kuongezeka kasi ya mapigo ya moyo (tachycardia) na dalili zinazofanana na msongo au wasiwasi mkubwa.

Mengine ni maumivu ya kifua, kubanwa kwa njia ya hewa na kuwa na pua inayotoa kamasi kila mara macho mekundu yanayotoa machozi.

Hali hii huweza kuandamana na aina tofauti za maumivu ya kichwa, uchovu, kuchanganyikiwa na hisia za kukereka.

Hali hii huweza kuandamana pia na kupoteza fahamu kwa sekunde moja au mbili, kujisikia vibaya kwenye njia ya chakula, kupata kiungulia, kuvimbiwa na hali ya kucheua maji makali ya tumboni (reflux).

Mizio inayozaliwa kutokana na mwili kushindwa kuhimili Histamine ni tofauti na ile inayoletwa na vyakula. Wakati mizio inayosababishwa na vyakula ni ya papo kwa papo baada tu ya kula, ile inayosababishwa na histamine huja taratibu huku ikiongezeka kidogo kidogo.

Mfano wa hali hii ni kama maji yaliyoko kwenye kikombe. Kikombe kinapokuwa kimejaa kabisa, tone moja la ziada la maji linatosha kufanya maji yaliyoko kwenye kikombe yaanze kumwagika.

Hata hivyo, maji yanapokuwa hayajajaa kwenye kikombe, kutahitajika kiasi kingi cha maji (histamine) kabla tukio la kumwagika kwa maji yaliyoko kwenye kikombe halijachochewa kutokea. Hali hii inasababisha utambuzi wa kuwa mwili hauna uwezo wa kuhimili histamine kuwa mgumu.

Kwa nyongeza, kushindwa kwa mwili kuhimili histamine kuna uhusiano wa karibu na ongezeko la kupindukia la bakteria kwenye utumbo mwembamba. Hii ina maana kwamba ukitibu tatizo hili la ongezeko la bakteria, basi moja kwa moja unaleta ufumbuzi katika tatizo la histamine.

Matabibu wengi wanaokumbatia mifumo tofauti ya tiba (integrative practiioners) wanaamini kuwa tatizo la mwili kushindwa kuhimili histamine, kimsingi linatokana na ongezeko kubwa lililopindukia mipaka la aina fulani za bakteria katika njia ya chakula.

Bakteria hawa hutengeneza histamine nyingi kutoka kwenye chakula ambacho hakikusagwa vema tumboni na kusababisha njia ya chakula kuwa na kiasi kikubwa cha kemikali hiyo.

Ongezeko hili kubwa la histamine huufanya uwezo wa mwili kuivunja na kuiondosha kuzidiwa. Hali hii huzidi kushusha uwezo wa mwili kuihimili histamine, hivyo kusababisha kujenga upinzani dhidi ya vyakula vyote vyenye histamine kwa wingi. Ulaji wa vyakula hivi moja kwa moja huzalisha dalili ambazo tunazioanisha na mizio.

Nini unachpaswa kufanya kama mwili wako hauwezi kuhimili histamine? Kwa kuwa vyakula vingi vina histamine na kwa baadhi ya watu bakteria walioko kwenye njia zao za chakula huzalisha kiasi kingi cha histamine kinachosababisha wawe na dalili za magonjwa zinazowakumba, tatizo hili kwa kweli linaweza kuwa ni changamoto kubwa katika kulipatia ufumbuzi.

Vyakula vilivyochachuliwa ni miongoni mwa vyakula vinavyoongeza uzito wa changamoto hii, ukizingatia kuwa hata bakteria wazuri walioko tumboni nao pia huzalisha histamine pale wanapokutana na mazingira ya uchachu.

Moja ya vipimo vyepesi vya kujua kama unakabiliwa na tatizo la mwili wako kutoweza kuhimili histamine ni kula vyakula vilivyochachuliwa.

Kwa mtu yeyote mwenye tatizo la mwili wake kushindwa kuhimili histamine, kuondoa vyakula vyenye histamine nyingi katika ulaji wake ni jambo la lazima, walau kwa muda fulani.

Baada ya hapo mgonjwa anaweza kuanza kula kiasi kidogo cha vyakula hivi. Hata hivyo athari ya histamine inatofautiana kati ya mtu na mtu. Wakati baadhi ya watu miili yao haiwezi kuvumilia kiasi chochote cha histamine, baadhi huathirika tu pale wanapokula vyakula vyenye kiasi kikubwa cha histamine.

Ili kuujengea mwili wako uwezo zaidi wa kuhimili histamine ni muhimu sana kuikarabati njia yako ya chakula ikiwa ni pamoja na kushughulikia matatizo yote yenye uhusiano na mfumo huo.

Unywaji wa maji wa kutosha ni moja ya njia za uhakika sana katika kudhibiti ongezeko kubwa la histamine na pia kukarabati njia ya chakula.

Kujenga mazoea ya kutumia tembe mbili hadi tano za vitunguu saumu kwa siku na kupunguza sana ulaji wa sukari na vyakula vya wanga iliyotokana na nafaka zilizokobolewa, ni mambo ambayo yatasaidia sana kupunguza wingi wa bakteria wabaya kwenye njia ya chakula.

Juma Kilagai ni mtaalamu wa kemia ya binadamu, anapatikana kwa simu 0754281131.
Mpya zaidi Nzee zaidi