https://monetag.com/?ref_id=TTIb Mulongo wawasimamisha kazi madaktari wawili na wauguzi watano kwa kusababisha kifo cha mjamzito Mwanza | Muungwana BLOG

Mulongo wawasimamisha kazi madaktari wawili na wauguzi watano kwa kusababisha kifo cha mjamzito Mwanza

Mkuu wa mkoa wa Mwanza Magesa Mulongo amewasimamisha kazi madaktari wawili na wauguzi watano wa Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Mwanza Sekou Toure, kutokana na uzembe unaodaiwa kusababisha kifo cha mama mzazi Pendo Masanja na watoto wake mapacha.

Tukio hilo linakuja ikiwa ni siku chache baada ya mapacha wengine kupoteza maisha wakati wa kuzaliwa katika hospitali ya wilaya ya nyamagana iliyopo Butimba jijini Mwanza kwa kile kinachoelezwa kuwa ni uzembe wa wauguzi pamoja na madaktari wa hospitali hiyo kushindwa kumhudumia kwa wakati mama mjamzito Suzan John machi 3 mwaka huu.

Mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza pia amewasimamisha kazi wauguzi wengine wawili wa hospitali ya Butimba ambao ni Nathan Bagaya na Edina Mwesiga,Daktari mmoja wa Hospitali hiyo Furaha Kingunge na dereva wa gari la kubeba wagonjwa ( AMBULANCE) Ghalib Hamad kwa kushindwa kumuongezea damu mama huyo mjamzito pendo masanja, huku akitangaza kuunda tume ya watu wanne ikiongozwa na mganga mkuu wa mkoa wa Mwanza Dk. Onesmo Rwakyendera kwa ajili ya kuanza uchunguzi dhidi ya watumishi hao.

Tume iliyoundwa na mkuu huyo wa mkoa wa Mwanza kuchunguza uzembe wa madaktari pamoja na watumishi wa hospitali hizo mbili za butimba na Sekou Toure, huenda ikaja na majawabu sahihi na ufumbuzi wa changamoto zinazopelekea kutokea kwa vifo vya watoto wachanga na akinamama wajawazito wakati wa kujifungua.