WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamepora Sh. milioni 13.4 za wakulima wa korosho kwa kutumia mapanga baada ya kuvamia ofisi za Chama cha Ushirika wa Wakulima kata za Marumba na Mbati (Mtiti Amcos) wilayani humu juzi, taarifa za kipelelezi zimedai.
Hata hivyo, uporaji huo uliofanyika juzi saa 4:00 asubuhi wakati viongozi wa chama hicho wakijiandaa kufanya malipo ya fedha hizo kwa wakulima baada ya kukusanyika, umegubikwa na utata baada ya maelezo ya tukio kupishana.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Rubery Mwombeji, alisema jana kuwa jeshi lake linawashikilia viongozi watatu wa Mtiti Amcos kwa ajili ya mahojiano ili kupata ukweli wa mazingira yaliyosababisha uporaji huo.
Kwa mujibu wa Kamanda Mwombeji, miongoni mwa maswali wanayotaka kujiridhisha kutoka kwa viongozi hao ni pamoja na uwapo wa mazingira mabovu ya utunzaji wa fedha hizo pamoja na kuchelewa kulipa wakulima tangu walipozichukua benki Ijumaa.
Jambo lingine ambalo linahitaji majibu kutoka kwa viongozi, alisema Kamishna Mwombeji, ni uwapo wa taarifa za kutatanisha za mazingira na jinsi fedha hizo zilivyoporwa.
Kamanda Mwombeji alisema katika mahojiano, baadhi ya viongozi wamedai kuwa majambazi waliwatisha kwa bunduki na mwingine akidai walitishwa kwa mapanga.
Viongozi watatu wanaoshikiliwa na Jeshi la Polisi Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma wakituhumiwa kula njama za kupora fedha hizo ni Mwenyekiti wa chama hicho, Ally Issa Njelu (60).
Wengine ni Karani Mkuu wa chama hicho, Abbas Ally Kaisi (38) na Karani Msaidizi wa chama hicho, Ally Kauga Mussa (40) ambaye pia ni mjumbe wa chama hicho, alisema Kamishna Mwombeji.
Taarifa kutoka kwa viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wakulima wa Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma zinaeleza kuwa viongozi wa chama hicho walipokea jumla ya Sh. milioni 103 Ijumaa kwa ajili ya malipo ya wakulima hao na kwenda kuzisambaza katika vituo vya malipo hayo.
Taarifa hiyo iliendelea kufafanua kuwa baada ya kusambaza fedha hizo na kufanya malipo kwa baadhi ya wakulima wa korosho, sh. milioni 13.4 zilisalia na kuhifadhiwa katika sefu ya kuhifadhia fedha ya
Mtiti Amcos.
Taarifa ilisema kiasi hicho ndicho kilichothibitika kuporwa na majambazi hao.
Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Juma Homera alisema viongozi wa chama hicho ni lazima warejeshe fedha hizo ili zilipwe kwa wakulima husika.
Aidha, Homera ameliagiza Jeshi la Polisi kuwasaka majambazi hao ili kubaini ukweli na minong’ono inayowatuhumu viongozi kuhusika katika tukio hilo.
Alisema matukio ya aina hiyo hayavumiliki.
Aidha, Homera aliwashutumu wakulima wilayani humu kwa kukaidi maelekezo ya serikali ya kufungua akaunti benki ili wawe wanaingiziwa fedha zao moja kwa moja, jambo ambalo lisingewashawishi majambazi hao kufanya uhalifu huo.
Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Tunduru, Issa Kambutu, pia alithibitisha kushikiliwa kwa viongozi wa chama chake na kueleza kuwa anaamini kuwa haki itatendeka ili kuwaondoa viongozi wake katika tuhuma hiyo.
Kambutu alisema yeye na viongozi wenzake katika Chama Kikuu wanawaamini viongozi hao kwani hadi linatokea tukio hilo, chama hicho kimekwisha chukua na kwenda kulipa wakulima wake zaidi ya Sh. bilioni moja zilizotokana na wakulima wa chama chao kukusanya na kuuza zaidi ya tani 300 za korosho.
