LICHA ya kufungiwa kucheza soka kwa msimu mmoja kwa kosa la kusaini mkataba wa kuichezea Mbeya City FC wakati huohuo akiwa bado katika mkataba wa kuichezea Tanzania Prisons, kiungo mshambulizi Mohamed Mkopi (mdogo wa Said Mkopi wa Mtibwa Sugar) mchezaji huyo mwenyeji wa Dar es Salaam bado ‘lulu’ na klabu nne za Dar zinapigana’ vikumbo’ kuhakikisha vinamsaini kwa ajili ya msimu ujao.
“Kwa msimu wote huu 2016/17 licha ya kufungiwa nimekuwa nikiendelea kufanya mazoezi Mbeya City, lakini bado nipo katika wakati mgumu wa kuamua ni klabu gani nitaichezea msimu ujao. Kuna timu wanataka nijiunge nazo na kuendelea kujifua huku wakiahidi kunipatia kila kitu ikiwemo kusaini mkataba lakini sijaitumikia City hata mechi moja hilo linaniumiza kwa kiasi fulani,” anaanza kusema Mkopi wakati nilipofanya naye mahojiano.
“Nilisaini mkataba wa mwaka mmoja kuichezea City na walinipa pesa yangu ‘keshi’ lakini nimeshindwa kuwatumikia kutokana na matatizo yaliyojitokeza wakati wa usajili wangu kutoka Prisons. City hawanipi mshahara baada ya hali hiyo kujitokeza.”
“Kuna timu ambazo zipo tayari kuwarudishia City pesa zao walizonipa wakati nasaini katika usajili wa dirisha kubwa mwaka uliopita. Kuna timu nne za Dar es Salaam zote zinanihitaji na nyingine kutoka mikoani ,” anasema Mkopi aliyezaliwa Oktoba 27, 1993.
Mkopi alifunga magoli 8 msimu uliopita akiwa Prisons ambayoalijiunga nayo kwa mkataba wa miaka miwili Juni 2015 akitokea Mtibwa Sugar FC ya Turiani, Morogoro ambayo ndiyo timu yake ya kwanza kuichezea katika ligi kuu ya Tanzania Bara.
Alijiunga na Mtibwa mwaka 2011 kutoka klabu ya Mtaani kwao Nondo Rangers ya Mwananyamala.
Baada ya kukutwa na matatizo ya kusaini mkataba wa kuichezea City wakati angali bado na mkataba wa kuichezea Prisons mchezaji huyo ameamua kusimamiwa hivi sasa.
“Kwa sasa nimefanikiwa kupata meneja ambaye atanisimamia.meneja wangu niMtanzania anayefahamika kwa jina la Mohamed bin Dau.”
