Mgambo saba, ni miongoni mwa watumishi tisa waliojeruhiwa baada ya mapambano na wafanyabiashara ndogondogo, maarufu kama wamachinga juzi, lakini sasa vita hiyo imehamia kwa viongozi wa kuchaguliwa dhidi ya watumishi wa Serikali wilayani Nyamagana.
Mmoja wa watumishi waliojeruhiwa ni mahututi baada ya kushambuliwa vikali na wamachinga wakati akishiriki kutekeleza operesheni ya kuwaondoa wafanyabiashara wanaopanga bidhaa zao pembezoni mwa barabara katika mji wa Buhongwa ulioko takriban kilomita 3.4 kutoka katikati ya jiji.
Mbunge wa Nyamagana, Stanslaus Mabula ameingia kwenye mzozo na kaimu mkuu wa wilaya hiyo, Dk Leonard Masale, akimtuhumu kuwaonea wamachinga na pia kukiuka agizo la Rais John Magufuli la kutaka wafanyabiashara hao waondolewe kwa utaratibu baada ya kutengewa maeneo yenye huduma muhimu.
Wakati Mabula akitoa tuhuma hizo, diwani wa Kata ya Buhongwa, Joseph Kabadi anashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kuhamasisha vurugu zilizosababisha watumishi wa jiji kujeruhiwa na gari kuharibiwa kwa kupopolewa mawe na machinga.
Buhongwa haimo katika orodha ya maeneo rasmi yaliyotengwa kwa ajili ya Machinga jijini Mwanza ambayo ni Makoroboi, Mlango Mmoja, Asante Moto, Tanganyika, Sahara, Dampo, Market Street, Nyegezi, Buzuruga, Mirongo na Liberty.
Lakini wafanyabiashara hao walilazimika kuanza kupanga bidhaa zao pembeni mwa barabara baada ya soko la eneo hilo kujaa na hivyo kuonekana kero kwa wapita njia na wamiliki wa maduka, hali iliyosababisha uongozi wa wilaya kuamua kuendesha operesheni ya kuwaondoa kuanzia Februari 17.
Operesheni hiyo, iliyoendeshwa kwa amri ya Dk Masale ambaye ametumia sura ya nane ya Sheria ya Mipango Miji Sura ya mwaka 2007, na Sheria ya Mazingira namba 25/1972, ilipingwa vikali na kuibua mapambano yaliyosababisha mgambo saba, ofisa mazingira na dereva wa jiji kulazwa Hospitali ya Sekou-Toure baada ya kushambuliwa na wamachinga.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi alisema hali ya mmoja wa mgambo hao, Ndaisabas Nicodemu (25), si nzuri baada ya kujeruhiwa katika tukio hilo lililohusisha mapambano ya kurushiana mawe.
“Gari moja la jiji lenye namba za usajili DFPA 2387 aina ya Sino limeharibiwa kwa kuvunjwa vioo,” alisema Kamanda Msangi.
Kamanda Msangi alisema mgambo mwingine, Alex Joseph (25) mkazi wa Isamilo amevunjika sehemu ya paja ya mguu wake wa kulia.
Wengine waliojeruhiwa ni Emmanuel Bigambo (37), mkazi wa Pasiansi aliyeumia kiuno, Asifiwe Andrea (33), mkazi wa Igogo na David Bakari (32) mkazi wa Nyamanoro, ambao wote wameumia goti la kulia.
Kamanda Msangi aliwataja majeruhi wengine kuwa ni ofisa mazingira wa jiji, Fanuel Kasenene (39), mkazi wa Nyegezi aliyejeruhiwa sehemu ya juu la jicho la kushoto na dereva wa jiji, Gharibu Ahamadi (32), mkazi wa Nyakato.
Mgambo wengine waliokumbana na hasira za machinga ni Zacharia Andrea (24), mkazi wa Mkolani na Surusi Joseph (21), mkazi wa Kiloleli ambao wote wameumia kwenye viwiko vya mikono yao ya kushoto.
Mbunge auvaa uongozi wa jiji
Vurugu hizo zimemfanya mbunge wa Nyamagana kumjia juu kaimu mkuu wa wilaya.
“Operesheni hii inapingana na agizo la Rais John Magufuli alilotoa Desemba 9 mwaka jana alipozuia wafanyabiashara hao wadogo kuondolewa katikati ya jiji bila ya kuandaliwa sehemu nyingine inayofaa,” alisema Mabula.
Katika agizo lake lililotengua Oparesheni Ondoa Wamachinga iliyoendeshwa na jiji kati ya Desemba 3 na 4 mwaka jana, Rais aliwaagiza viongozi wa jiji kuwashirikisha na kuwatengea wafanyabiashara hao maeneo ya kuhamia yanayofikika na yenye miundombinu kabla ya kuwahamisha.
“Licha ya kuwa nje ya jiji, kule Buhongwa hakuna eneo maalumu lililotengwa kwa ajili ya Machinga. Sasa wanahamishwa ili waende wapi?” alihoji Mabula juzi.
Mbunge huyo alimwomba Rais Magufuli kuingilia kati suala hilo kuepuka madhara zaidi huku akiahidi kuendelea kuwaunga mkono wamachinga aliodai wanaonewa na mamlaka za Serikali za mitaa.
Kaimu mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Mariam Ukwaju alisema operesheni hiyo ni halali kwa mujibu wa sheria, kanuni na maelekezo ya Serikali kupitia kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Tamisemi), George Simbachawene.
Katika agizo lake, Simbachawene aliagiza mamlaka za serikali za mitaa kuwaondoa wamachinga waliotumia vibaya amri ya Rais Magufuli kwa kuvamia na kupanga bidhaa kwenye njia za waenda kwa miguu na maeneo mengine yasiyoruhusiwa.
Dk Masale hakupatikana kuzungumzia tuhuma za mbunge huyo baada ya simu yake ya kiganjani kuita bila kupokelewa kutwa nzima ya jana.
Umeshawahi Kufikiria Kupata Gari la Bure bila Kulipa Chochote, Basi hii Kampuni ya Cars From Japan Wanakupa Nafasi Hiyo ...
Chakufanya ni Kubofya Link hapo chini na Ufate Maelekezo ya Jinsi ya Kuweza Kuwa Mshindi wa Gari hilo..
Chakufanya ni Kubofya Link hapo chini na Ufate Maelekezo ya Jinsi ya Kuweza Kuwa Mshindi wa Gari hilo..
Kisha Jisajili kwa Kuweka Jina na Email Yako... USIWE NA WASIWASI HUDUMA HII NI SALAMA KABISA..

