Je unajua sababu za wachezaji wa Afrika Mashariki kushindwa kutoboa Ulaya?

Nchi za Afrika Mashariki bado zinalili wachezaji wake wakacheze soka la kulipwa nje ya Afrika, lakini kwa wenzetu Afrika Magharibi kitu kama hiki sio tatizo kabisa kwao, wanawachezaji wa kutosha tena kwenye klabu na ligi zenye majina makubwa duniani. Mataifa kama Ghana, Nigeria, Mali, Senegal, Cameroon tayari yamefanikiwa katika hilo.

Kiungo wa Tottenham na timu ya taifa ya Kenya Victor Wanyama amezitaja sababu kadhaa ambazo zinapekelea wachezaji wa Afrika Mashariki kushindwa kutoka kwenda kucheza nje ya Afrika.

Kuridhika mapema na kukata tama ni miongoni mwa sababu zilizotajwa na Wanyama. Amesema hata yeye kuna wakati alikaribia kukata tamaa lakini alipambana kwa sababu alikuwa akijua kuna wakati utafika mambo yatakaa sawa.

“Wachezaji wa huku tunakata tama mapema na kuridhika haraka, kwa sababu unakuta mchezaji lengo lake ni kwenda kucheza Mali akifika pale anatosheka badala kujituma ili afike mbali zaidi.”

“Kuchelewa kuoneshwa kwa ligi zetu kumechangia wachezaji wengi wa ukanda wa Afrika Mashariki kuchelewa kutoka kwenda nje ukilinganisha na mataifa mengine ya Afrika hasa Afrika Magharibi. Lakini ujio wa Azam na DSTV umefanya ligi ziwe zinafuatiliwa na kuwarahisishia kazi mascaut kuona wachezaji.”

Ilifika wakati hata yeye alitaka kukata tamaa    

Nikiwa Ubelgiji kuna wakati mambo yalikuwa magumu sana kwa sababu nilienda kule kabla sijafikisha miaka 18 kwa hiyo sikuwanza kucheza moja kwa moja, nilikuwa nafanya mazoezi tu lakini sichezi mechi. Nikawa nawapigia simu nyumbani nataka kurudi lakini walikuwa wananizuia kwa kuniambia kama nina nyumba nirudi lakini kama sina niendelee kuka hukohuko.

Nikawa najaribu kumpigia simu hadi ndugu yangu Mariga akawa ananiambia nisirudi basi nikaamua kupambana nikaendelea.

Kwa nini timu za ukanda wa Afrika Mashariki hazifanyi vizuri?

Kuto cheza mechi nyingi za kirafiki kwa sababu unakuta mnacheza mechi moja halafu mnasubiri mechi za kufuzu ndio mcheze tena, lakini sasa hivi wameanza kujua nini tatizo na wameanza kupanga mechi nyingi za kirafiki kwa hiyo tunakuja juu kidogo.

Changamoto kubwa tunayokutana nayo ni utofauti wa ligi kwa mfano kwa sasa ligi za Ulaya zimeisha lakini huku nyumani bado ligi zinaendelea kwa hiyo mkienda kwenye timu ya taifa kuna kuwa na level tofauti ya fitness kwa sababu wachezaji wengine walikuwa likizo , wengine ligi ilikuwa inaendelea kwa hiyo huo ndio ugumu.

Ukiangalia Kenya sasa hivi ligi inaendelea, halafu sisi ligi imemalizika, wakati mimi narudi kwenye ligi wao ndio wanaenda likizo sasa mkikutana kwenye timu ya taifa unakuta wengine level ya fitness inatofautiana wengine wanakuwa chini wengine juu.

Wachezaji wa Tanzania anaowafahamu

Nimewaona wachezaji wengi wa Tanzania kama Samatta, Ngasa, na wengine sijui kama bado wanaendelea kucheza kama Kaseja nimemuona pia akicheza.

Kuhusu ubaguzi wa rangi

Kuhusu ubaguzi wa rangi inauma sana kwa sababu mwisho wa siku sisi sote ni binadamu halafu rangi ni kitu ambacho hakihusiani na mpira. Mpira ni mchezo unaoleta watu pamoja wafahamiane unaleta upendo na amani.

Ubaguzi wa rangi unavyoletwa kwenye mpira huwa una haribu lakini FIFA wanajitahidi kupiga vita japo ni vigumu kuisha ila naamini ipo siku itakwisha.

Ushauri kwa wachezaji wa Tanzania

Samatta amefungua njia kwa hapa Tanzania kwa hiyo wachezaji wengine wakipata nafasi wasikate tamaa, msimu huu Samatta amefanya vizuri sana msimu ujao kama akifanya vizuri kama msimu huu au zaidi basi atakuwa na nafasi ya kucheza timu yoyote kubwa.