Mayanja awatuliza Simba kuhusu sare

WAKATI mabingwa wa Kombe la FA, Simba ya jijini Dar es Salaam wakilazimishwa suluhu dhidi ya Mlandege ya Zanzibar katika mechi ya kirafiki iliyofanyika juzi usiku, siri ya kutopangwa kwa washambuliaji Emmanuel Okwi na John Bocco katika mchezo huo imebainika.

Taarifa kutoka katika benchi la ufundi la Simba zinasema kuwa lengo la kutowapanga washambuliaji hao wawili ni kuwapumzisha kwa ajili ya kuwasubiri mahasimu wao Yanga ambao watakutana katika mechi ya kuwania Ngao ya Jamii itakayofanyika Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Chanzo hicho kilisema kuwa washambuliaji hao "wametumika" zaidi tangu walipojiunga na kambi jijini Johannesburg, Afrika Kusini na sasa wanahitaji kuongeza nguvu ya kupambana na Yanga katika mchezo huo wa ufunguzi wa msimu mpya wa ligi.

"Tuliwapumzisha. Tunataka wawe na nguvu zaidi kwa ajili ya kuwamaliza Yanga, hiyo ni moja ya siri ya kutowatumia jana (juzi), pia leo (jana) jioni Bocco anatarajiwa kurejea kwenye mazoezi ya pamoja na wenzake baada ya kuumia katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar," alisema kiongozi mmoja.

Wakati huo huo, Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja amewaodoa hofu mashabiki baada ya timu yao kushindwa kupata ushindi katika mchezo huo wa juzi.

Mayanja alisema kuwa kiufundi mchezo huo umewasaidia kuendelea kuwafahamu wachezaji wao na matokeo ya sare yaliyopatikana yamesababishwa nyota wao kucheza kwa tahadhari.

"Ni kweli suala la ushambuliaji na umaliziaji halijakaa vizuri kwa upande wa timu yetu, ila ninawaondoa hofu mashabiki na wanachama wa Simba, tuko vizuri na watatuona tukirejea Dar es Salaam," alisema kocha huyo wa zamani wa Coastal Union na Kagera Sugar zote za hapa nchini.

Aliongeza kuwa jana timu hiyo ilitarajia kuendelea na mazoezi yake ya mwisho na leo usiku inatarajia kushuka tena dimbani kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Gulion utakaofanyika kwenye Uwanja wa Amaan.
Mpya zaidi Nzee zaidi