GEORGE LWANDAMINA.
KITAELEWEKA, hiyo ni kauli ya Kocha Mkuu wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, George Lwandamina baada ya kikosi chake kupata mfumo rasmi ambao watautumia katika mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya mahasimu wao Simba itakayofanyika Jumatano kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana baada ya mazoezi ya asubuhi, Lwandamina, alisema kuwa tayari ameandaa mifumo tofauti ambayo ameifanyia kazi kwa siku zote tangu kikosi hicho kilipoanza maandalizi kwa ajili ya msimu mpya.
"Tumefanya mazoezi mbalimbali na kutengeneza mifumo zaidi ya mmoja, lakini mfumo wa 4-4-2 ndio tutakaoanza nao Jumatano," alisema Lwandamina.
Kocha huyo alisema kuwa mfumo huo utatoa nafasi kwa washambuliaji Ibrahim Ajibu na Donald Ngoma kuanza kwa pamoja na hilo limeonekana hata kwenye mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea.
“Itategemea na aina ya timu au aina timu tunayocheza nayo, tutakua tukibadilika kulingana na uwezo wa wapinzani wetu, nashukuru kambi inaenda vizuri na wachezaji wanaonekana kushika kile ambacho ninakielekeza na hii inatia moyo,” Lwandamina alisema.
Naye Meneja wa timu hiyo, Hafidh Saleh, aliiambia gazeti hili kuwa hakuna majeruhi kwenye timu hiyo na wamepanga kurejea jijini Jumanne tayari kwa mchezo huo utakaofanyika kuanzia saa 10:00 jioni.
Meneja huyo alisema kuwa hawatacheza mechi nyingine ya kirafiki na sasa kilichobakia ni kurekebisha makosa mchache ya kiufundi ambayo waliyabaini kwenye michezo waliyocheza ya kujipima nguvu.
Yanga imekuwa ikifanyia mazoezi mifumo ya 4-3-3 na 3-4-2-1 ambapo huu utaifanya timu hiyo kujaza viungo katikati na kuacha mshambuliaji mmoja mbele.
