JAJI Mkuu Prof. Ibrahim Juma, amesema mabaraza ya kata ni muhimu katika kusimamia utoaji wa haki kwa wananchi na kwamba endapo yatawezeshwa na kuelimishwa, yatapunguza msongamano wa kesi zisizo za lazima katika mahakama za mwanzo na wilaya.
Profesa Juma alisema hayo jana kwenye ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Igunga, mkoani Tabora alipokuwa akizungumza na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo katika ziara yake ya kikazi aliyoianza Tabora.
Alisema mabaraza ya kata yana umuhimu katika kusimamia utoaji wa haki kwa wananchi na kwamba yakiwezeshwa yatapunguza msongamano wa mashauri mbalimbali katika mahakama za mwanzo na wilaya.
Aidha, kutokana na umuhimu huo, aliwaagiza mahakimu wa mahakama za mwanzo na wilaya nchini, kuendelea kuboresha utendaji wa kazi za idara ya Mahakama kwa kutenga muda maalum wa kutoa elimu kwa wananchi ili kutambua kikamilifu haki zao.
Aidha, Prof. Juma alisisitiza kwamba kazi ya mahakama ina changamoto nyingi kwa kuwa baadhi ya wananchi hawatambui namna ya kudai haki zao katika mahakama, hivyo ni wajibu wa mahakimu kutenga muda maalumu wa kutoa elimu kwa wananchi.
Alisema endapo elimu itaendelea kutolewa kwa wananchi, ikiwamo kwa njia ya mabango na kukemea vitendo vya rushwa, itasaidia kupunguza msongamano wa kesi zisizo za lazima katika mahakama.
Jaji Mkuu alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa wananchi kutambua kuwa haki yoyote inapotafutwa, inapaswa kuanzia nyumbani mwao kwa kuwa yapo baadhi ya mambo wanaweza kuyasuluhisha pasipo kuyafikisha mahakamani.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Igunga, John Mwaipopo, alimweleza Jaji Mkuu kuwa Igunga ina wakazi 420,933 sawa na ongezeko la wastani wa asilimia 2.9 kwa mwaka.
Alisema kutokana na idadi kubwa ya wananchi, zinahitajika huduma za kimahakama kwa kuwa wilaya inazo mahakama za mwanzo 10 na mahakama moja ya wilaya wakati kiutawala zipo tarafa 4, kata 35 na vijiji 119.
Mwaipopo alisema kutokana na hali hiyo, baadhi ya wananchi wamekuwa wakitembea umbali mrefu kutafuta huduma za mahakama, hivyo kumwomba Jaji Mkuu kujengwa mahakama za mwanzo katika kata zote 35 na kama hakuna uwezekano, zijengwe angalau 15.