Chuo Kikuu watoa ombi hili kwa Rais Magufuli


CHUO Kikuu cha Waislamu Morogoro (MUM), kimemuomba Rais John Magufuli kukisaidia kurejesha kiwanja chake cha ukubwa wa ekari 400 kilichopo eneo la Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Ofisa Uhusiano wa MUM kwa kushirikiana na Taasisi ya Maendeleo ya Waislamu (MDF), Ngaja Mchele, alisema eneo hilo limeanza kuingiliwa na watu ilihali wameshaanza taratibu za kujenga chuo cha biashara.

'Tunamuomba Rais Magufuli ashughulikie suala hili la Kigamboni na kufanyike uchunguzi na watakaobainika kusababisha mtafaruku huu wachukuliwe hatua kukomesha dhuluma ili ujenzi uanze haraka kwa faida ya Watanzania wote," alisema.

Alisema kuwapo kwa fitna zinazofanywa na watu wasiojulikana ambao waling'oa jiwe la msingi lililowekwa, kunachelewesha kuanza kwa ujenzi wake.

"Kitendo hiki kimetusikitisha sana, kimekusudia kuchelewesha harakati zetu za ujenzi ilihali MDF na chuo wana nyaraka zote zinazothibitisha uhalali wa umiliki wa eneo hilo," alisema Mchele.

Aidha, Mchele aliwataka waislamu wote nchini na viongozi waliopata taharuki kutokana na kusambaa kwa taarifa hizo, kuendelea kuwa watulivu wakati uongozi wa chuo ukilishughulikia suala hilo.

Hata hivyo, Julai 6, 2016 Rais Magufuli aliahidi kusaidia Waislamu kurudishia mali walizonyang'anywa ama kurubuniwa, wakati akihutubia katika Baraza la Eid el Fitri, jijini Dar es Salaam.

Miezi mitano baadaye, Kamati Maalumu iliyoundwa na Shehe Mkuu wa Tanzania, Mufti Abubakar bin Zubeir kuhakiki mali hizo, iliwasilisha taarifa ya awali ikibainisha changamoto kadhaa.

Akizungumza Dar es Salaam Novemba 23, mwaka huo, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Shehe Abubakary Ally, alisema wamebaini changamoto kadhaa, ikiwa ni pamoja na baadhi ya mali kutohakikiwa kutokana na kukosekana kwa taarifa sahihi kama ni za Baraza la Waislamu (Bakwata).

Alisema baadhi ya vitu walivyochunguza kwenye ripoti hiyo ni mikataba, viwanja, majengo na mali zingine za Baraza, hivyo baada ya Mufti kuisoma ataeleza kilichojiri kupitia vyombo vya habari.

Na Septemba 12, mwaka jana Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alikutana na Mufti Zubeir na tume iliyoundwa kuhakiki mali za Waislamu jijini Dar es Salaam, Waziri Lukuvi alipokea ripoti kutoka kwa Mufti ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli.