Mkoa wa Kilimanjaro washindwa kufikia malengo yake


Moshi. Mkoa wa Kilimanjaro umeshindwa kufikia malengo katika bajeti yake ya mwaka 2018/19 baada ya kukusanya Sh8.04 bilioni katika vyanzo vyake vya mapato wakati ilipanga kukusanya na kutumia Sh21.3 bilioni.

Halmashauri ya Mwanga ndio iliyoshika nafasi ya kwanza kwa kukusanya mapato mengi ikilinganisha na halmashauri nyingine.

Hayo yameelezwa jana Februari 28, 2018 na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira wakati akitoa taarifa hiyo katika kikao maalumu cha bajeti ya mkoa huo, huku akizitaka

halmashauri zote kuongeza juhudi na kutafuta mbinu mpya itakayowezesha kusaidia kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Mkuu wa mkoa huyo amesema makusanyo yameshuka kutokana na halmashauri nyingi kushindwa kurudisha asilimia 20 kwa ajili ya vijiji sambamba na asilimia nne kwa ajili ya wanawake na walemavu ambao wanaishi katika Serikali za vijiji ambazo ndizo vyanzo mojawapo vya mapato.

"Kwa kweli hii ni aibu mkiangalia wenyewe katika makadirio ya Sh21.34 bilioni hadi kufikia Sh8.04 bilioni ni aibu kubwa. Wakurugenzi kwa hili mnapaswa kuwajibika na kuhakikisha mnazipatia haki zao Serikali za vijiji na mitaa asilimia ili zione umuhimu wa kukusanya mapato,” amesema.

“Haiwezekani halmashauri ya kijjiji na mitaa ikusanye mapato halafu hawapati stahiki zao, halafu mtegemee awamu nyingine kupata mapato ya ndani. Badilikeni na mhakikishe mnawapatia haki zao.”

Ameipongeza Halmashauri ya Mwanga kwa kukusanya asilimia 58 ya makusanyo yao ukilinganisha na halmashauri zingine mkoani humo.

"Naipongeza pamoja na changamoto za askari walizoziainisha, lakini wameongoza kwa kukusanya mapato mengi

ukilinganisha na halmashauri nyingine. Ninaomba halmashauri zote zifanye mapitio ya vyanzo vyao vya mapato na kujiwekea mikakati ya kuboresha ukusanyaji mapato,” amesema.

Mpya zaidi Nzee zaidi