WATU WATANO WAFARIKI DUNIA NA WENGINE KUJERUHIWA BAADA YA TOYOTA COASTER KUPATA AJALI LUSHOTO.

 


Watu watano wamefariki dunia na wengine nane kujeruhiwa baada ya Toyota Coaster, namba T.151 DMC, kuacha barabara na kutumbukia bondeni eneo la Vuga, Lushoto. Ajali hiyo imetokea leo Agosti 18, 2026, majira ya saa 7:30 mchana.



Kwa mujibu wa kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga Almachius Mchunguzi, amesema gari hilo lilikuwa likitokea Tanga Mjini kuelekea Ngwashi, likiendeshwa na Ally Dione.


Amesema Waliofariki ni wanaume wawili, wanawake wawili na mtoto mchanga anayekadiriwa kuwa na umri wa miezi sita ambao majina yao bado hayajatambuliwa.


Watu wengine nane wamejeruhiwa na wamelazwa katika Kituo cha Afya Soni, Lushoto, kwa ajili ya matibabu. Miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto.


Uchunguzi wa awali umebaini kuwa ajali hiyo inadaiwa kusababishwa na uzembe wa dereva, aliyeshindwa kulimudu gari na kuacha barabara na kutumbukia bondeni.


Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi kubaini chanzo na mazingira ya ajali hiyo. Aidha, limewataka madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuwa makini ili kuepusha ajali zinazoweza kuzuilika.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi