Mahakama ya ICC imemuondolea makamu wa rais wa zamani wa nchini DRC Jean Pierre Bemba makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu ambayo alikuwa amepatikana nayo.
Alikuwa anatumikia kifungo cha miaka 18 jela kutokana na makosa hayo.
Bemba alikuwa amepatikana na hatia mwezi Machi mwaka 2016 kwa makosa ya uhalifu, uliotokea katika nchi jirani ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, kati ya mwaka 2002 na 2003 na akahukumiwa 21 Juni.
Mahakama hiyo imetoa uamuzi huo kufuatia rufaa aliyoiwasilisha kupinga hukumu hiyo.
Uamuzi wa mahakama umepokelewa kwa shangwe na wafuasi wake waliokuwepo ukumbi wa mahakama, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
