Serikali imeshauriwa kuwashirikisha waajiri wakati wa kuandaa mitaala ya elimu katika vyuo vya ufundi nchini ili vijana wanaohitimu mafunzo kwenye vyuo hivyo wakidhi mahitaji ya waajiri hali ambayo pia itawarahisishia vijana kupata ajira kirahisi.
Ushauri huo umetolewa na mratibu wa ukuzaji ujuzi wa shirika la kazi duniani, ilo, nchini Tanzania, Herbert William Mkali wakati akizungumza na vijana wanaotekeleza mradi wa Stride ambao unaendeshwa na shirika la Technoserve ukilenga kuwawezesha vijana kutambua fursa za kujiingizia kipato zilizopo kwenye maeneo yao.
Meneja mkazi wa shirika la Technoserve nchini Tanzania, Mwasapile Kajimbwa amesema mradi wa Stride ambao umeanza kutekelezwa katika mikoa ya Mbeya na Songwe, una lengo la kuwafanya vijana wa kitanzania waachane na fikra za kuajiriwa na badala yake watumie fursa zilizopo kwenye maeneo yao kujiingizia kipato.
Akizungumza kwa niaba ya katibu tawala wa mkoa wa Mbeya, afisa uchumi na uwezeshaji ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mbeya, Said Juma Madito amesema serikali kupitia halmashauri zake, imewaweka mazingira mazuri kwa vijana na akina mama kwa kuwapatia mikopo ya riba nafuu ili waweze kupata mitaji inayowawezesha kutumia fursa zinazopatikana kwenye maeneo yao kujikwamua kiuchumi.