Kansela Angela Merkel wa Ujerumani amekutana na Rais Nana Akufo-Addo wa Ghana mjini Accra, katika siku ya pili ya ziara ya Afrika Magharibi, inayolenga kuimarisha maendeleo ya kiuchumi na kudhibiti uhamiaji haramu.
Uimarishaji wa maendeleo ya kiuchumi barani Afrika ni suala la kipaumbele kwenye ajenda ya sera ya kigeni ya Ujerumani, ambapo Merkel alisema katika ujumbe wa vidio kabla ya kuanza ziara yake hii kwamba ni muhimu kwa mataifa mengi ya Afrika kwa sababu kuna vijana wengi sana barani humo wanaotafuta ajira na mafunzo.
Harakati hizo za kidiplomasia barani Afrika, ambazo zimehusisha ziara nchini Mali, Niger, Ethiopia na Misri kwa kansela huyo wa Ujerumani mwaka 2016, zinaweza kuwa muhimu kwa mustakabali wa kisiasa wa Merkel kwa sababu zinaunda msingi wa mkakati wake wa kukabiliana na visababishi vya uhamiaji na ukimbizi.
Merkel amepoteza uugwaji mkono wa kisiasa tangu alipochukuwa uamuzi wa kuwakaribisha mamia kwa maelfu ya wahamiaji nchini Ujerumani, na chama chake cha Christian Democratic Union, CDU, kiko katika nafasi dhaifu sana kuliko ilivyowahi kutokea katika historia yake ya miongo sita.
Akiwa nchini Senegal, alizungumzia haja ya kukabiliana na uhamiaji haramu na wanaofanya biashara ya usafirishaji binadamu.
"Hatuwezi kuwa washiriki wa wasafirishaji haramu wa watu. Hatuweza kukaa na kuangalia watu wakihatarisha maisha yao katika bahari ya Mediterrania. Ndiyo maana ziara hii na ujumbe nilioambatana nao ni muhimu," alisema Merkel katika mkutano wa pamoja na rais wa Senegal, Macky Sall.
