Rais wa Marekani Donald Trump ameikosoa China kwa kuhujumu jitihada zake na Korea Kaskazini, wakati kuna malalamiko kuhusu maendeleo ya kuharibu silaha za nyuklia za Korea Kaskazini.
Kupitia ujumbe wa Twitter alisema hakuna sababu ya kutoendelea tena na mazoezi ya kijeshi na Korea Kusini ambayo yamekuwa yakiikasirisha Korea Kaskazini.
Siku zilizopita waziri wake wa ulinzi alisema mazoezi ya kijeshi yanaweza kuendelea.
China imeikosoa Marekani kwa kuilaumu kuhusu uhusiano wake na Korea Kaskazini.
Mkutano kati ya Trump na kiongozi wa Korea kaskazini Kim Jong-un mwezi Juni ulikamilika kwa ahadi kutoka Korea Kaskazini kufanya kazi katika kuharibu silaha za nyuklia kwenye rasi na Korea.
Baadaye Trump alitangaza kuwa hakukuwa tena na tisho kutoka Korea Kaskazini.
Lakini tangu wakati huo waangalizi wengi wanasema kuwa Korea Kaskazini haifanyi hima katika kuharibu maeneo yake ya kurushia makombora.
Kwa nini anailaumu China?
Kwenye matamshi yake kupitia Twitter, Bw Trump anasema Korea Kaskazini iko chini ya shinikizo kutoka China kwa sababu ya mvutano wa kibiashara kati ya Marekani na serikali ya China.
China ndiyo mshirika pekee wa Korea Kaskazini na inatajwa kuwa na ushawishi mkubwa kwenye maamuzi yake. China pia ndiye mshindani mkubwa wa Marekani na wa muda mrefu eneo hilo.
