Mume Auawa na Wananchi Baada ya Kumuua Mke Wake

Mkazi  wa kijiji cha Kinku  tarafa ya Mungaa wilaya Ikungi , Singida, Editha Kanisi (49) ameuawa kwa  kukatwa kwa  kisu cha kukatia majani, (mundu) shingoni na kichwani na mume wake Joseph Wilbroad (53).

Baada ya Joseph kufanya mauaji hayo wananchi wenye hasira kali nao walimshambulia kwa silaha na kumuua.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana   Agosti 16 Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoa wa Singida, ACP Sweetbert  Njewike alisema tukio hilo limefanyika  Agosti 15 mwaka huu usiku saa mbili huko katika kijiji cha Kinku.

Alisema kuwa tukio hilo lilitokea  usiku wakati  wanandoa hao wakijiandaa kulala na uliibuka mzozo mkali baina yao huku kila mmoja akimtuhumu mwenzake kuwa si mwaminifu kwenye ndoa.

“Kila mmoja alimtuhumu mwenzake kutokuwa mwaminifu katika ndoa yao,”alisema.

Akifafanua zaidi alisema malumbano hayo yalisababisha mwanaume kuchukua kisu cha kukatia majani kiitwacho mundu na kumkata mke wake shingoni na kichwani.

Alisema Editha alijaribu kukimbia lakini alipotoka nje ya nyumba yao alianguka chini na kufariki dunia papo hapo.

 “Watoto wao baada ya kuona mama yao kaanguka chini, walianza kupiga kelele za kuomba msaada na majirani walifika mara moja kwenye eneo la tukio na wakamwomba Joseph afungue mlango,” alisema Kamanda huyo

"Joseph alikaidi kufungua mlango na ndipo walipouvunja kwa nguvu.Walipofanikiwa kumkamata Joseph,walimpiga kwa silaha za jadi na kusababisha kifo chake,”aliongeza.

Alisema uchunguzi zaidi na msako mkali unaendelea kuwasaka waliohusika na mauaji ya Joseph.