Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imetoa ufafanuzi juu ya upatikanaji wa chaneli zilizopo kwenye orodha ya zile za bure katika visimbuzi vya Digitek, Continental, Ting na Startimes.
Kupitia tangazo lililotolewa na mamlaka hiyo leo Jumamosi Agosti 25, 2018 linaeleza kuwa ili kupata huduma ya chaneli hizo, wananchi wanatakiwa kutumia antena zenye muundo wa mwiba wa samaki.
Baadhi ya mikoa iliyotajwa na mamlaka hiyo ni Dar es Salaam, Tanga, Mwanza, Singida, Kagera, Morogoro, Mbeya, Arusha Mara, Shinyanga, Tabora, Rukwa na Songea.
Akieleza sababu za kutumia antena hizo, mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa TCRA, Semu Mwakyanjala amesema hilo ni suala la kiufundi kwa ajili ya ubora na muonekano.
“Ni kweli hilo tangazo ni la TCRA na huu ni mfumo wa mitambo ambayo ni teknolojia ya aina yake,” amesema.
Amebainisha kuwa kutokana na asili ya ardhi ya Tanzania ya baadhi ya maeneo kuwa na miinuko na mabonde, wamebaini kuwa kuna baadhi ya maeneo yanafaa kwa antena hizo.
Julai 6, 2018, naibu waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye alitembelea TCRA na kuagiza kuchukuliwa hatua kwa wamiliki wa ving’amuzi kwa kukiuka masharti, kwa kuonyesha chaneli zilizopo kwenye orodha ya zile za bure kinyume cha matakwa ya leseni zao.
