Serikali ya JPM yafikia lengo la kujenga viwanda kwa asilimia 61


WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema hadi kufikia Juni, 2018 jumla ya viwanda 1,596 vimejengwa ambapo ni sawa na asilimia 61.4 ya lengo la kujenga viwanda 2,600 hadi Desemba 31, 2018 ikiwa ni utekelezaji wa agizo la ujenzi wa viwanda 100 katika kila mkoa.

Ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 27, 2018) wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 34 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT), kwa niaba ya Rais Dkt. John Magufuli. Mkutano huo umefanyika katika ukumbi wa Jakaya Mrisho Kikwete, jijini Dodoma.

Waziri Mkuu amesema kuwa viwanda hivyo vimejengwa kupitia agizo la Waziri wa Nchi TAMISEMI kwamba kila Mkoa ujenge viwanda 100.

Amesema tathmini ya utekelezaji wa mkakati wa Serikali kuelekea uchumi wa viwanda, inaonesha kwamba mpaka sasa jumla ya hekta 367,077 zimetengwa katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa ajili ya viwanda vikubwa, viwanda vya kati na viwanda vidogo.

“Nitoe wito kwenu kwamba mwendelee kupiga hatua nyingine mbele zaidi katika hili, tujue katika hekta hizo zilizotajwa ni kiasi gani kimerasimishwa kwa viwanda vipi, bidhaa zipi zinazalishwa, hali ya miundombinu ikoje na kuna mikakati gani ya kuiendeleza. Pia tufahamu ni ajira ngapi zilizozalishwa kutokana na uanzishwaji wa viwanda hivyo.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewaagiza viongozi na wasimamizi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kutekeleza majukumu yao kikamilifu ili kuwawezesha wananchi kushiriki katika kubuni na kusimamia miradi ya maendeleo na kuibua fursa za uwekezaji.

Mpya zaidi Nzee zaidi