10/11/2018

Familia ya MO yafanya dua


FAMILIA ya Mfanyabishara maarufu nchini, Mohammed Dewji, imesema inafanya  sala na dua kuhakikisha ndugu yao anapatikana akiwa mzima.

Msemaji wa klabu ya Simba, Haji Manara, ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwa niaba ya familia na bodi  ya wakurugenzi ya Simba.

Amesema kikao walichokutana leo kati ya familia na bodi hiyo wameamua kumuombea lakini pia kuliachia Jeshi la Polisi jukumu la kutoa taarifa zote ninazohusika na tukio hilo.

Pia amesema wameshtushwa na kusikitishwa na taarifa za uzushi zilizotolewa na mitandao ya kijamii kuwa Mo amepatika.

“Familia na Bodi ya wakurugenzi ya klabu ya Simba na wanachama kwa ujumla tuendelee na dua za kuhakikisha ndugu yetu anapatikana akiwa mzima na wale wote waliohusika wanakamatwa ili  kuchukuliwa hatua," amesema.

Pia amesema jana walikuwa na Mo kwenye kikao cha Bodi ya Wakurugenzi ya Simba kujadili maendeleo ya klabu hiyi na mara ya mwisho kuwasiliana naye ilikuwa ni saa 5:00 usiku.