Wananchi wa Kijiji cha Mwenge, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Vijijini, wamedaiwa kuchoma nyumba 20 za watuhumiwa wa mauaji ya wanawake katika kijiji hicho, baada ya kudai kuachiwa huru na Jeshi la Polisi na baadaye kudaiwa kujigamba uraiani kuwa mwenye pesa hawezi kufungwa jela.
Tukio hilo lilitokea juzi majira ya saa nne asubuhi katika kijiji hicho, baada ya wananchi kuchukizwa na vitendo vya watuhumiwa hao kuachiwa huru, wakati wakituhumiwa kutekeleza mauaji ya wanawake wanaotuhumiwa kujihusisha na imani za kishirikina.
Akizungumza jana na Nipashe, Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Paschal Chuma, alisema watuhumiwa hao waliachiwa huru kwa maelezo kuwa ushahidi wa kuwatia hatiani umekosekana, jambo ambalo wananchi hawakuridhika nalo na kuamua kujichukulia sheria mkononi.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Mchema Bundala, Lole Yusufu, Malenga Rozalia, Charles Nziku na Paulo Futumo, wanne kati yao walifanikiwa kukimbia na kubaki mmoja Yusufu ambaye alinusurika kifo baada ya kuokolewa na Jeshi la Polisi waliofika eneo la tukio kutuliza fujo.
“Baada ya watuhumiwa hao wanne kukimbia na mmoja kuokolewa na Jeshi la Polisi, ndipo wananchi wakaelekeza hasira zao kwenda kuchoma moto nyumba zao zipatazo 20, kwa madai hawataki kuishi na wauaji,” alisema Chuma.
Diwani wa Kata ya Mwenge, Edward Maganga, alisema awali baada ya kusikia watuhumiwa hao wameachiwa huru, alikwenda kuonana na uongozi wa Jeshi la Polisi na kupewa majibu kuwa wameachiwa huru baada ya ushahidi kukosekana na kueleza kuwa katika tukio hilo hakuna kifo.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Shinyanga (ACP), Alchelaus Mutalemwa, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kutolea ufafanuzi kuwa watuhumiwa waliachiwa kwa mujibu wa kifungu namba 61(A) cha sheria ya mashtaka, baada ya ushahidi kutokamilika.
Alitoa wito kwa wananchi mkoani Shinyanga, wanapohitajika kwenda kutoa ushahidi mahakamani kuhusu matukio ya uhalifu, wawe wanahudhuria kwa kuwa mtuhumiwa hawezi kutiwa hatiani kama ushahidi haujajitosheleza hali inayofanya wananchi kulitupia lawama Jeshi la Polisi bila sababu za msingi.
Wakati wa mkutano uliopita wa Bunge la Bajeti, ilielezwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kuwa katika kipindi cha kuanzia mwezi Julai, 2017 hadi Machi mwaka huu, jumla ya watu 117 (wazee/vikongwe) waliuawa nchini.
Kati yao, wanawake 26 na wanaume 91 na matukio hayo yalitokea katika mikoa ya Arusha (6), Dodoma (10), Geita (9), Iringa (1), Kagera (10), Katavi (3), Kigoma (1), Mara (2), Mbeya (7), Morogoro (2), Mwanza (9), Njombe (5), Rukwa (10), Shinyanga (3), Simiyu (5), Singida (6), Songwe (12) na Tabora (25).
