Rais TFF: Hatuuzi ligi yetu kwa bei chee


Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia amesema kuwa shirikisho hilo haliko tayari kuuza chapa ya ligi kuu kwa mdhamini mwenye kiwango kidogo cha pesa kwakuwa thamani ya ligi ni kubwa.

Suala hilo limekuja baada ya kuibuka kwa maswali mengi kuhusu udhamini mkuu wa ligi kuu Tanzania bara (TPL) ambayo mpaka sasa ikielekea katikati ya msimu ikiwa haina mdhamini mkuu aliyetangazwa kama ilivyoahidiwa na TFF mwanzoni mwa msimu.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na kipindi cha Kipenga cha East Africa Radio kinachoruka saa mbili usiku, Rais huyo wa TFF amesema,

" Mwanzoni mdhamini mkuu alisema ataendelea lakini baada ya majadiliano kiwango kikashuka, wakasema wameambiwa wabane. Sisi hatuwezi kukubali kumpa mdhamini mkuu wa ligi kwa kiasi kidogo kama kile, na sisi tukamwambia hapana ".

" Kwahiyo tunaendelea kutafuta wadhamini wengine kwa kushirikiana na bodi ya ligi lakini pia tunaendelea na mazungumzo na mdhamini mkuu wa awali, kwa kiasi chake kile ili awe mdhamini mwenza, asiwe mdhamini mkuu ", ameongeza.

 " Ligi ya Uingereza hivyohivyo kulikuwa na mvutano kuhusu thamani ya ligi, mpaka leo ligi haina mdhamini mkuu, kwanini Tanzania mnalazimisha twende kwenye udhamini mkuu wakati thamani yetu tunaona ni kubwa sisi?, tutakuja kumpa yule ambaye tunadhani kwamba atatupa hela inayolingana na thamani yetu ".
Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia