Halmashauri za Dodoma kubanwa mapato


MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, ameziagiza halmashauri zote kuandaa taarifa inayoonyesha matumizi ya makusanyo ya mapato yanayokusanywa kwa miaka mitatu.

Mahenge alitoa agizo hilo alipokuwa akizungumza na wataalamu kutoka idara mbalimbali kwenye ziara ya kukagua miradi ya uwekezaji wa majengo pamoja kukutana na wananchi kuhusu kutatua kero za ardhi jijini hapa.

Alisema pamoja na makusanyo kuwa mazuri, lakini ni muhimu ikaandaliwa taarifa ya matumizi yanayotokana na vyanzo vya mapato.

"Naomba mnitengenezee jedwali inayoonyesha vyanzo vyote ambavyo mmekusanya mapato na muonyeshe kwa miaka mitatu mmepata kiasi gani? Maana msipofanya hivyo mnaweza kujiona mmekusanya mapato mengi, lakini kwenye matumizi mkajikuta siyo mazuri.

"Ni muhimu sasa kwa halmashauri zote mkajipanga kwa hilo katika ukusanyaji pamoja na kufahamu matumizi," alisema.
Aidha, alizitaka halmashauri hizo kuhakikisha zinakuwa na mtizamo wa kuingalia miaka 100 mbele katika umiliki na upangaji wa maeneo, ili kuondokana na kero ya ardhi na wananchi.

"Haina maana pekee kujivunia na haya maendeleo ya uwekezaji tuliyonayo yanayoendelea kwa hivi sasa kama vile uwanja, stendi soko la kisasa ujenzi uliopo Nzuguni bali tuangalie na maeneo mengine kuweka uwekezaji huo," alisema.

Kadhalika, aliwataka watendaji wa idara mbalimbali kufanya kazi zao pamoja na wananchi kwa lengo la kutatua kero zao badala ya kukaa ofisini kusubiri wawafikie.

Dk. Mahenge alilitaka Jeshi la Polisi mkoani humo kuhakikisha linalinda amani kwa wananchi hususan katika kipindi ambacho serikali inaondoa kero za ardhi kwa wananchi wa Dodoma.

Mpya zaidi Nzee zaidi

Popular Items

Kilimo cha Bamia