Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), imefanya upasuaji mkubwa wa aina yake wa kuunganisha mifupa ya fuvu na kutengeneza taya kwa wagonjwa tisa.
Upasuaji huo unagharimu Sh. milioni saba kwa mgonjwa mmoja akitibiwa hapa nchini, wakati nje ya nchi ungegharimu zaidi ya Sh. milioni 60.
Daktari bingwa wa upasuaji wa taya, kinywa na uso kutoka Hospitali ya MNH, Daud Shabani, aliwaambia waandishi wa habari jana wakati wakifanya upasuaji huo.
Alisema walianzisha kambi maalum kwa ajili ya kufanya upasuaji huo unaochukua saa saba baada ya kupata wageni kutoka Hospitali ya Kansas City na Chuo Kikuu cha Missouri, Marekani.
Alisema wataalamu hao walikuja kwa ajili ya kuwaongezea ujuzi, utaalamu pamoja na kuwapatia msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya Sh. milioni 250 ambavyo vitawasaidia kutoa huduma kwa wagonjwa wenye matatizo hayo.
“Tumefanikiwa kufanya upasuaji wa kibingwa wa kuunganisha mifupa ya fuvu kwa mgonjwa aliyepata ajali na sura yake kuharibika na kuirudisha katika hali yake,” alisema.
Aliongeza: “Wiki yote hii tunafanya upasuaji na leo (jana) tunafaya upasuaji wa kumtoa mgonjwa taya iliyoathirika na maradhi na kumjengea mpya kwa kutumia chuma maalum na pia kuvuna mfupa wake kutoka kwenye kiuno kuongezea taya jipya ili baadaye tumwekee meno aendelee na maisha,” alisema.
Aidha, alisema changamoto kubwa katika kutoa huduma hiyo ni upatikanaji wa vyuma hivyo maalum kwa kuwa gharama yake ni kati ya Sh. milioni nne hadi sita.
“Mgonjwa huyo kama angeenda nje ya nchi kutibiwa angelazimika kulipa kati ya Dola za Marekani 20,000 hadi 28,000 ambazo ni zaidi ya Sh. milioni 60 kwa mgonjwa mmoja, lakini hapa kwetu tunatumia Sh. milioni saba kwa mgonjwa mmoja,” alisema.
Aidha, Dk. Shaban alisema tatizo la ugonjwa huo ni kubwa na linawakumba watu wote na kwamba hata watoto wenye umri wa miaka mitatu wamekumbwa na matatizo kama hayo na wameshawahi kuwatibu.
Dk. Shaban alisema wagonjwa wengi wenye tatizo la uvimbe wa taya wanatoka kwenye mikoa inayopitiwa na bonde la ufa kama Mbeya, Tabora, Shinyanga hadi Kanda ya Ziwa.
Alisema hakuna utafiti uliofanyika, lakini wanahisi kutakuwa na chembechembe kwenye udongo, chakula na maji yanayotoka katika bonde hilo na kuchangia tatizo hilo.
“Hili bado halijathibitishwa sana nihisia kutokana na uzoefu wetu. Tatizo ni kubwa kwa Watanzania na kwa sasa wodi zimejaa wagonjwa hao na hata tunapokwenda mkoani kutoa huduma tunakutana nao wengi ingawa takwimu halisi hatuna, lakini ni wengi na tiba yake ni upasuaji tu,” alisema.
Aidha, Dk. Shaban alisema wataendelea kufanya upasuaji huo hata kama wataalamu hao wataondoka kwa kuwa vifaa wamepatiwa na wataalamu wako 13 wenye uzoefu katika ugonjwa huo.
