Makala: Matukio 10 ya kiburudani yaliyotikisa mwaka 2018

Hatimaye mwaka 2018 ndio huo unaelekea mwishoni kabisa, umekuwa na mambo mengi kwa kiasi chake kwenye kila nyanja.

Kwa upande wa burudani ni mengi yamejiri na kutikisa vilivyo. Haya ni matukio 10 yaliyotawala upande wa Burudani kwa mwaka huu.

1. Kifo cha Masogange

Ni binti mrembo aliyejulikana kama Agnes Gerald kutoka mkoani Mbeya. Mara baada ya kutokea kwenye video ya muimbaji Belle 9 'Masogange' akiwa kama video vixen ndipo alipata umaarufu mkubwa na kuanza kutumia jina hilo.

Hata hivyo Masogange alianza kuonekana kwenye video ya wimbo wa Mwana FA  na AY inayokwenda kwa jina la Nangoja Ageuke iliyotoka mwaka 2008. Baada ya kuonekana kwenye video za wasanii kadhaa na kujizolea umaarufu mkubwa aliamua kuingia kwenye filamu. 

Hatimaye April 20, 2018 katika Hospitali ya Mama Ngoma iliyopo Mwenge, Dar es Salaam, Masonge alifariki dunia akiwa ni mama wa mtoto mmoja na kuzikwa April 23, 2018 mkoani Mbeya.

Mwili wa Masogange uliagwa April 22, 2018 katika viwanja vya  Leader Club, Da es Salaam. Katika misa/ibada hiyo iliyohudhuriwa na idadi kubwa ya wasanii kulitokea matukio mawili ambayo  yalijadiliwa sana kwenye mitandao ya kijamii.

Mosi; Kukutana kwa Alikiba na Diamond, hawa ni wasanii wakubwa Tanzania ni washindani kwenye muziki wao. Kitendo cha Alikiba kumgeuzia kiganja wakati wakusalimia kiliweza kujadili sana. 

Pili;  Ni muigizaji Rammy Galis ambaye alikuwa ni mpenzi wa Masogange kuzimia na kubebwa na watu lakini aliendelea kung'ang'ania na kushikilia kitambaa chake cha mkononi, wengi walidai kitu hicho hakiwezekani.

Kabla ya umauti kumfika, April 03, 2018 Masogange aliachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam baada ya kukutwa na hatia ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroine na Oxazepam (alilipa faini).

2. Harusi ya Alikiba

Alfajiri ya April 19, 2018 (alhamisi) Alikiba alifunga ndoa na Mrembo Aminah Rikesh Ahmed huko mjini Mombasa nchini Kenya. Kama ulikuwa hujui siku kama hiyo miaka mingi iliyopita ndipo na wazazi wa muimbaji huyo walifunga ndoa.

Baada ya Mombasa, shughuli nzima ikahamia Dar es Salaam ambapo Aprili 29, 2018 kwenye Hoteli ya Serena maharusi hao walijumuika na watu wao wa karibu na wageni waalikwa.

Harusi hiyo ilikuwa ikijadiliwa sana mtandaoni na wengi waliweza kuishuhudia moja kwa moja kupitia Azam TV. 

Miongoni mwa watu maarufu waliohudhuria ni pamoja na Mke wa Rais Mstaafu, Mama Salma Kikwete, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamisi Kigwangalla na wengineo. 

Pia siku hiyo ndio kwa mara ya kwanza Alikiba alitambulisha kinywanji chake cha Mofaya ambacho pia kwa mara ya kwanza kilionekana kwenye wimbo wake uitwao Mvumo wa Radi kwa lengo la kukitangaza (product replacement).

Pia ndani ya mwezi huo (April 22, 2018) mdogo wake na Alikiba, Abdu Kiba naye alifunga ndoa ambapo walifanya sherehe ya harusi pamoja ndani ya Serena Hotel kama nilivyotangulia kueleza. 

3. Video ya Faragha ya Nandy na Bill Nass

Kwa kipindi kirefu walikuwa wakizushiwa kuwepo mapenzini lakini walikuwa wakitupilia mbali tetesi hizo  zilizowanyima usingizi wapenda udaku.

Hatimaye mchana wa April 12, 2018 ikabainika ni kweli Nandy na Bill Nass waliwahi kuwa wapenzi baada ya video yao wakiwa faragha kuvuja mtandaoni.

Hadi kufika Aprili 17, 2018 suala hilo lilifika bungeni ambapo Mbunge wa Ulanga, Goodluck Mlingwa aliyehoji jinsi gani serikali imejipanga kupambana na wasanii wa muziki  anaosambaza lugha za matusi. 
 

Akijibu swali hilo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alisema siku moja kabla Diamond Platnumz alikamatwa kwa kosa hilo na kutoa agizo kwa polisi kumkatamata na Nandy.

Hata hivyo siku mbili mbele (April 19, 2018)  Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) iliwaita Nandy na Diamond kwa ajili ya mahojiano ambapo wote walikiri makosa yao na kupewa nafasi ya kuomba radhi.

Diamond alijikuta kwenye sekeseke hilo kufuatia pia kuvuja kwa video yake ya faragha akiwa na mzazi mwenzie, Hamisa Mobetto na wanawake mwingine mmoja ambaye hakufahamika. 

Hilo pia halikumuacha salama Hamisa Mobetto kwani naye pamoja na Irene Uwoya, July 19, 2018 waliitwa na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania  (TCRA) na kuwataka kuomba radhi kwa kosa la kuweka picha za utupu mtandaoni ambapo walitii hilo.

4. Kuteuliwa kwa Jokate Mwegelo 

Mrembo huyo aliyekuwa Miss Tanzania namba mbili mwaka 2006 alitambulika vema akiwa kama Mwanamitindo, msanii wa muziki na filamu, pia mjariamali.

Mchana wa July 28, 2018 Rais John Magufuli alimteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe. Uteuzi wake ulikuwa baada ya mrembo huyo kususia mitandao ya kijamii tangu April 20, 2018 hadi kipindi cha uteuzi kwa sababu ambazo yeye binafsi hajawahi kuziweka wazi.

Kabla ya uteuzi huo Jokate aliwahi kuwa Kaimu Katibu wa Hamasa na Chipukizi wa Umoja wa Vijana Chama cha Mapinduzi (UVCCM), kabla ya March 25, 2018 Mwenyekiti wa umoja huo, Kheri Denis James kutangaza kutenguliwa kwa uteuzi wake. 

Ijumaa ya August 03, 2018 ndipo Jokate aliapishwa na Rais wa Jahmuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kuanza kutumikia nafasi hiyo. 

Uteuzi wa Jokate ulipokelewa kwa shangwe na vijana wengi kutokana na nguvu ya ushawishi alionayo kwao kwa kipindi kirefu.

Utakumbuka May 2017 Jokate Mwegelo alichaguliwa na jarida la Forbes Africa kuwa miongoni mwa vijana 50 wenye umri chini ya miaka 30 waliopata mafanikio katika sekta mbalimbali.  

5. Kifo cha Mzee Mjuto

Jina alilopewa na wazazi wake ni Amri Athuman, sanaa ya maigizo na uchekeshaji ikampa jina la Mzee Majuto. Alifanikiwa kuvunja mbavu za mashabiki wake kwa miaka ya mtoto hadi mtu mzima (zaidi ya 18).

Usiku wa Augusti 08, 2018 ndipo alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) mara baada ya kutoka nchini India.

Kabla ya umauti kumfika, Mzee Majuto alipatiwa matibabu ndani na nje ya nchi ambapo May 04, 2018 alisafirishwa kwa ajili ya matibabu nchini India na June 22, 2018 alirejea nchini. 

Mzee Majuto aliagwa August 09, 2018 kwenye viwanja vya Karimjee, Dar es Salaam na tukio hilo kuhudhuriwa na Rais John Magufuli, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete na viongozi wengine, alizikwa siku iliyofuata mkoani Tanga. 

6. Muendelezo wa Wasafi Festival, Miss Tanzania na  SZIFF

Tunaweza kusema kwa mwaka huu kulikuwa ni kupatwa kwa wapenda Burudani mara baada ya kurejea kwa kishindo kwa Wasafi Festival na shindano la Miss Tanzania. 

Tamasha la Wasafi chini ya Diamond Platnumz na wasanii wote wa WCB liliwahi kufanyika na kusitishwa na mwaka huu limerejea ambapo limeweza kupita kwenye mikoa ya Mtwara, Morogoro, Iringa, Mwanza, Sumbawaga na Visiwani Zanzibar.

Hapo awali WCB waliwahi kufanya Wasafi Festival lakini si kwa ukubwa wa sasa. Utakumbuka tena walifanya kitu kinaitwa Wasafi Beach Party, hii ikiwa ni katika jitihada za kuandaa show zao wenyewe.

Tuakiachana na hilo, pia mwaka huu yamereja mashindano ya Miss Tanzania baada ya kutofanyika kwa miaka miwili.

Utakumbuka baada ya kufanyika mwaka 2016 na mrembo Diana Edward kuibuka mshindi yalisimama hadi yalipokuja kufanyika mwaka huu na mrembo Queen Elizabeth kuibuka mshindi. 

Pia mwaka huu ugawaji wa tuzo za filamu za Sinema Zetu International Film Festival Awards (SZIFF) uliendelea ambapo ulifanyika April 01, 2018 kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. 

Tuzo hizo zilikuwa na jumla ya vipengele 18 huku kimoja kikiwa cha People Choice na kukamilisha jumla ya vipengele 19,  mgeni rasmi alikuwa Rais Mstaafu Jakaya  Kikwete.

Muigizaji Gabo Zigamba aliondoka na tuzo tano, huku Wema Sepetu akijinyakulia mbili.

Kitendo cha Diamond na Hamisa Mobetto kuonekana pamoja jukwaani ni kitu kilichowavutia wengi kwa sababu ndio ilikuwa mara ya kwanza kuoneka pamoja baada kupata mtoto na kuibua figisufigisu (drama) za hapa na pale.

Pia ujio wa muigizaji wa tamthilia kutoka nchini India, Pritika Rao ulinogesha vilivyo tuzo hizo na kuweka historia ya aina yake kwa wapenda burudani nchini.
(namba hii imekuwa na matukio matatu kwa sababu ni yenye kujirudia). 

7. Kifo cha Patrick 

Mtoto Patrick Dickson aliwavutia wengi kwenye mitandao ya kijamii, ni mtoto wa msanii wa filamu Bongo, Rose Alphonce Nungu maarufu kama Mona Love.

Patrick alifariki July 03, 2018  nchini Kenya akipatiwa matibabu ambapo alikuwa akisumbuliwa zaidi na maradhi ya miguu hali iliyo mpelekea kushindwa kutembea na mara kadhaa alifanyiwa upasuaji. 

Masikini, ni Patrick maarufu kama Patda Smart Boy, habari za kifo chake zilizombaa zaidi mtandaoni. BBC Swahili kupitia mtandao wao walichapisha habari kuhusu 'malaika' huyo aliyeonekana kuja kufanya vizuri kwenye uimbaji na mitindo. 

8. Diamond na BASATA 

Kwa mwaka huu Diamond Platnumz amekuwa na wakati mgumu zaidi kwa upande wake na Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) baada ya nyimbo zake kadhaa kufungiwa. 

February 28, 2018 Mamlaka ya Mawasiliana nchini (TCRA) ilipokea orodha ya nyimbo 15 zisizokuwa na maadili kutoka Basata ambazo zilifungiwa na kutotakiwa kuchezwa kwenye vyombo vya habari.

Kati ya hizo ni nyimbo mbili za Diamond ambazo ni Waka na Hallelujah. Kufuatia hatua hiyo Diamond alijikuta 'akivutana' kimaneno na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Juliana Shonza.

Katika mahojiano na kituo cha Radio Times FM, Mach 19, 2018, Diamond alimshtumu Shonza kuwa anafanya uonevu kwa kufungia nyimbo zake na hana uelewa kuhusu sana. 

Kutokana na hilo kitu hicho cha Radio ilipofika March 22, 2018 kiliandikiwa barua na TCRA kikitakiwa kuwasilisha kipindi cha The Playlist kilichorushwa tarehe hiyo kwa uchunguzi zaidi.

Baada ya hilo kutulia Diamond akajikuta tena Basata, safari hii lilikuwa ni suala la msanii Rich Mavoko aliyekuwa akitaka kujitoa kwenye lebo hiyo kwa kile kinachodaiwa ni mkataba wa kinyonyaji ingawa hilo limekuwa likakanushwa na pande zote mbili. 

August 09, 2018 kuliibuka taarifa kuwa Rich Mavoko ameshinda kesi ya kujitoa WCB ndipo zikaanza safari za muimbaji huyo na uongozi wa lebo hiyo Basata kwa lengo la kusuluhishi. hata hivyo hadi mwisho jitihada hizo hazikufua dafu.

Baada ya hilo kupita, ilipofika November 12, 2018 wimbo wa Rayvanny na Diamond 'Mwanza' ulifungiwa na Basata kutokana kukiuka maadili. Ilipofika December 18, 2018 wasanii hao wakafungiwa kutojihusisha na sanaa kwa muda usiojulikana kutokana na kuendelea kuutumia wimbo huo. 

9. Babu  Seya na Papii Kocha jukwaani tena

Kwa zaidi ya miaka 13 mashabiki walikuwa wamekosa burudani ya wasanii wao waliotamba vilivyo miaka ya nyuma. Ni  Nguza Viking ‘Babu Seya’  na mwanaye Johnson Nguza ‘Papii Kocha’ waliokuwa wakitumikia kifungo jela.

Kwa mara ya kwanza March 10, 2018 Babu Seya na Papi Kocha walifanya show ya pamoja ndani ya ukumbi wa King Solomon Hall, Dar es Salaam.

Utakumbuka December 09, 2017 wakati Tanganyika ikihadhimisha miaka 56 ya Uhuru, Rais Dkt. John Magufuli alitoa msahama kwa wasanii hao.

Mwaka huu ndipo waliweza kuonekana vilivyo uraiani na kwenye matukio mbalimbali ya sanaa. January 02, 2018 walifika Ikulu kwa ajili ya kumshukuru Rais Magufuli, pia April 19, 2018 walialikwa Bungeni na  Spika wa Bunge, Job Ndugai.

10. Lulu uraiani 

Utakumbuka November 13, 2017 muigizaji wa filamu Bongo, Elizabeth Michael ‘Lulu’ alihukumiwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kukutwa na hatia ya kumuua aliyekuwa muigizaji mwenzake, Steven Kanumba bila kukusudia.

Usiku wa May 12, 2018 zikaanza kusambaa stori kuwa Lulu ameonekana uraiani, siku iliyofuta Jeshi la Magereza lilieleza kuwa Lulu amebadilishiwa adhabu na atatumikia kifungo cha nje kwa amri ya Mahakama Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam.

Hatimaye Jumatatu ya November 12, 2018 Lulu akamaliza kutumikia kifungo chake cha nje na kuwa raia huru.

Kesi ya Lulu ilianza kunguruma tangu mwaka 2012 ambapo ndipo kifo cha Kanumba kilitokea, mwaka 2013 alitoka kwa dhamana hadi pale ilipokuja tena kusikilizwa mwaka 2017 na hukumu kutolewa.

Imeandikwa na Peter Akaro 
Mpya zaidi Nzee zaidi