Fahamu kuhusu tatizo la kukosa hamu ya tendo la ndoa

Ndugu zangu leo napenda tulijadili tatizo la kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa. Tutajadili sababu zinasababisha mwanaume kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa, madhara yanayotokana na hali hiyo na kisha kuona ni nini cha kufanya ili kuongeza hamu ya kufanya tendo la ndoa au kuongeza hamu.

Bahati nzuri ni kwamba kuna mambo unayoweza kuyafanya kupunguza ukubwa wa tatizo hili au kuliondoa kabisa. Watu wengine wanamini kuwa hamu ya kufanya tendo la ndoa inapungua kadri umri wa mwanamme unavyoongezeka.

Wakati ni kweli kwamba hilo huwatokea wengi, SIYO LAZIMA kwamba hamu ya kufanya mapenzi ipungue umri unapoongezeka. Kuna idadi kubwa tu ya wanaume ambao hamu yao ya kufanya tendo la ndoa imebaki vilevile hata umri wao ulipokuwa mkubwa kabisa. Kwanza tuanze kwa kutazama ukubwa wa tatizo hili.

Ukubwa wa tatizo la kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa
Wanaume wengi hawapendi kulizungumzia tatizo hili waziwazi na hata wanawake pia. Pamoja na kwamba tatizo hili halijitokezi sana kwa wanaume ukilinganisha na wanawake, inakadiriwa kuwa asilimia 15 hadi 16 ya wanaume wana tatizo hili, kwa lugha nyepesi kuna mwanamme mmoja mwenye tatizo hili baina ya kila wanaume sita au saba.

Idadi ya wanawake wenye tatizo hili ni mara mbili ya wanaume. Tatizo hili huwakera zaidi wanaume kuliko wanawake kwa sababu wanaume huchukulia urijali kama sehemu ya ukamilifu wa mwanamme na hunyongea wanapoona wana mapungufu kuhusu mambo ya mapenzi, tofauti kabisa na wanawake. Idadi ya wanaume wanaoridhika kuishi na tatizo hili ni ndogo sana ukilinganisha na ile ya wanawake. Hata hivyo tatizo la mwanaume kukosa hamu ya kufanya mapenzi limebainika kuwa ndilo linaloongoza katika kuleta migogoro ya unyumba kuliko matatizo mengine yote.

Utajuaje Kama Una Tatizo La Kukosa Hamu Ya Kufanya Tendo La Ndoa?
Tatizo hili halitokei ghafla kama vile umelala halafu ghafla asubuhi unaamka una mafua, la hasha. Ni kitu kinachotekea pole pole na pengine mwenyewe usijigundue. Sanasana pima mwenendo wako wa masuala ya mapenzi kwa mwaka uliopita au miezi kadhaa iliyopita.

Vile vile kutofanya tendo la ndoa kwa kipindi fulani haimaanishi kutokuwa na hamu ya kufanya mapenzi, pengine una hamu thabiti lakini mazingira hayakukuruhusu. Lakini iwapo hakuna kikwazo cho chote na upo na mwenzi wako halafu inapita wiki bila kufanya tendo la ndoa au unalifanya tendo hilo mara moja au mbili tu kwa mwezi, inabidi uanze kujiuliza maswali.

Lakini ieleweke pia kuwa kuhesabu umefanya tendo la ndoa mara ngapi katika kipindi fulani si kipimo pekee cha tatizo hili. Mawazo yako kwa ujumla kuhusu tendo hili ni muhimu pia – jinsi unavyolichukulia na kuliwazia tendo hili kabla, wakati wa tendo na baada ya kumaliza tendo ni muhimu katika kujipima.

Viashiria vingine vyaweza kuwa: kumtomasa mkeo mkiwa ndani tu – chumbani na si penginepo. Iwapo tendo hili unalifanya pale tu mwezi wako anapokuanza na huwa unalifanya kama mazoea bila kuwa na mawazo ya kushiriki kikamilifu.

Kama humwazii mpenzi wako anapokuwa hayupo kwamba angekuwapo ungeweza kufanya naye tendo la ndoa. Vitu hivi kama vinakutokea basi kuna dalili za kuwa unakosa hamu ya kufanya tendo la ndoa na kwamba inabidi utafute suluhisho.

Sababu za mwanamme kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa

Tatizo la kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa kwa mwanamme linaweza kusababishwa na vitu vingi sana. Sababu hizo zinaweza kuwa za kimaumbile au kisaikolojia au za mchanganyiko wa vitu hivyo viwili. Hebu tuone baadhi ya vyanzo vya tatizo hili.

Mahusiano baina ya mwanamme na mwanamke
Matatizo ya mahusiano kati ya mwanamme na mwanamke yana mchango mkubwa sana katika kusababisha tatizo la kukosa hamu ya mapenzi. Jee, unapata raha na una amani katika mahusiano yako na mpenzi wako? Huna wasiwasiwo wote na mahusiano yenu? Haya ni maswali ya msingi ya kujiuliza.

Kama mahusiano yako na mpenzi wako yamekuwa ya miaka mingi sana, unaweza kuwa umemzoea mno mkeo kiasi kwamba ukaanza kukosa hamu ya kufanya naye tendo la ndoa. Hili nalo hutokea mara nyingi.

Kama kuna mambo yanasababisha tendo la ndoa lisifanyike kwa urahisi, ufanisi na kufurahia, hamu ya kufanya tendo hilo inaweza kupungua. Kwa mfano, kama mwanamme unawahi kufika kileleni au una matatizo ya jongoo wako kupanda mtungi, tendo zima la ndoa halitakuwa la kukufurahisha sana hivyo unaweza kupoteza hamu ya kulifanya. Hebu fikiria tunda linalokufurahisha sana ukilila, ukilikosa kwa siku kadhaa, utalikumbuka na kulitafuta lakini ambalo halikufurahishi sana ukilila hutalikumbuka na kulitafuta.

Mawazo mengi na uchovu
Matatizo ya kikazi na hadhi yako kazini vyaweza kuchangia. Kama unabenwa sana kazini na kujiona hutimizi kazi yako ipasavyo au kama unachoka sana kazini unaweza pia kukosa hamu ya kufanya mapenzi urudipo nyumbani. Kukosa mpango mzuri wa shughuli zako za kila siku na kujaribu kulazimisha kufanya mapenzi katikati ya ratiba yako iliyojaa. Mahusiano ya kimapenzi yanataka yatengewe muda wake na unaotosha.

 Msongo wa mawazo
Msongo wa mawazo (depression) unatofautiana na kukosa raha au kujisikia si mtu wa thamani kwa kipindi kifupi. Msongo wa mawazo ni ugonjwa wa hali ya kuwa na mawazo makali ya muda mrefu ya kukukosesha raha kutokana na kujisikia si mtu wa thamani au kukosa starehe katika vitu ulivyozoea kuvifanya na kukufurahisha hapo zamani. Mawazo ya namna hii huathiri mwenendo wako wa maisha yako pamoja na matamanio yako ya kimapenzi.

Matumizi ya madawa na pombe
Matumizi ya baadhi ya madawa na unywaji wa pombe wa kupindukia huweza kuleta tatizo hili la kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa.

Umri kuwa mkubwa
Homoni ya msingi sana kuhusiana na masuala ya mapenzi huitwa testosterone. Kwa mwanammme homoni hii hutolewa kwa kiwango kikubwa na korodani na kwa mwanamke hutolewa na ovari. Homoni ikipungua katika mwili wa binadamu, humfanya apoteze hamu ya kufanya tendo la ndoa. Kiwango cha testosterone katika mwili wa mwanamme hupungua kwa asilimia 1-2 kila mwaka kadri mwanamme anvyozidi kuwa na umri mkubwa. Kiwango cha testosterone kikishuka sana katika mwili wa mwanamme huyu humfanya asiwe na nguvu, ashindwe kutuliza mawazo kwenye jambo alifanyalo na apoteze hamu ya kufanya mapenzi.

Matatizo katika mfumo wa homoni
Tumeshaona kwamba upungufu wa homoni inayoitwa testosterone unasababisha kukosa hamu ya kufanya tendo la ndoa. Matatizo mengine katika mfumo wa homoni huchangia tatizo hili. Kama thyroid haitoi homoni za kutosha, tatizo hili huweza kutokea ingawa mchango wa thyroid katika tatizo hili ni mdogo sana. Thyroid ni kiungo cha kuzalisha homoni kilichopo katika eneo la shingo.
Tatizo hili linaweza kutokea pale homoni zinapozalisha kitu kinachitwa prolactin kwa kiwango kikubwa mno na kukisambaza ndani ya mfumo wa damu. Hali hii kiutaalamu huitwa hyperprolactinaemia.

Matatizo ya kiafya
Matatizo ya kiafya ya muda mrefu husababisha kupungua kwa hamu ya kufanya tendo la ndoa. Matatizo ya moyo ya muda mrefu, kuwa na kisukari kwa muda mrefu, kansa ya muda mrefu na hali ya kuwa na unene wa kuzidi kiwango ni baadhi tu ya matatizo yanayochangia tatizo hili.