Loading...

5/15/2019

Waziri Kakunda ataja vipaumbele vya bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/20


Wizara ya Viwanda na Biashara imesema mwelekeo na vipaumbele vya bajeti kwa mwaka wa fedha 2019/20 ni pamoja na kuifanya sekta binafsi kuwa injini ya uchumi.

Hayo yalisemwa na Waziri wa Viwanda na Biashara, Joseph Kakunda, alipokuwa akisoma hotuba ya bajeti yake bungeni ambapo bunge limuidhinishie Sh. bilioni 100.38, kiasi ambacho ni pungufu ta Sh bilioni 48.88 ikilinganishwa na bajeti inayoisha.

Kakunda alisema Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki na wezeshi ili kuhakikisha wadau wote wanatoa mchango unaohitajika katika ujenzi wa uchumi wa Taifa.

Alisema pamoja na mazingira rafiki ya uwekezaji katika viwanda na biashara, utekelezaji wa mpango wa kuboresha mazingira ya biashara (blue print) unaangaliwa kuwa sehemu ya tiba ya changamoto ambazo zinaitatiza sekta binafsi.

“Hivyo ni mategemeo ya Serikali kuona sekta binafsi inachukua nafasi yake na kuchangamkia fursa zilizopo za kuzalisha na kutoa huduma ikiwa ni hatua muhimu ya kutambua jitihada za Serikali katika kutatua matatizo wanayokabiliana nayo,” alisema.

Kakunda aliitaja miradi ya kimkakati kuelekea ujenzi wa viwanda mama kuwa ni pamoja na Mchuchuma na chuma cha Liganga.

Alisema miradi hiyo inatekelezwa na Kampuni ya Tanzania China International Mineral Resources Limited ambayo ni ya ubia kati ya Serikali kupitia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) na Schuan Hongda Group ya China.

Kipaumbele kingine alikitaja kuwa ni kufufua kiwanda cha matairi Arusha, maarufu General Tyre kilichokuwa GTEA na utafiti wa kina juu ya ufufuaji huo umeshakamilika.

“Baada ya matangazo kutolewa kupitia tovuti ya NDC, wawekezaji mbalimbali wamejitokeza ikiwamo Kampuni ya Sayinvest Overseas (T) Limited ambayo imeonesha nia ya dhati ya kuwekeza katika uzalishaji matairi nchini.

“Aidha Serikali itaendeleza mradi wa mashamba ya mpira mikoa ya Morogoro na Tanga ambapo NDC imepanda miche takribani 85,250 katika eneo la wazi katika shamba la Kalunga na hadi kufikia Desemba 2018 hekta 155 zilikuwa tayari zimepandwa.

“Mradi mwingine ni uchimbaji wa magadi soda katika Bonde la Engaruka, Wilaya ya Monduli unaohusu kiwanda cha kuzalisha magadi hayo tani milioni moja kwa mwaka kwa matumizi ya viwanda vya dawa, vioo na sabuni,” alisema.
Loading...