Masoko ya Madini yaingiza Tsh. Bilioni 4 tangu kufunguliwa Machi mwaka huu


Masoko ya Madini nchini yameingiza zaidi ya Sh bilioni 4 katika kipindi cha siku 75 tangu yaanze kufunguliwa Machi, mwaka huu.

Kufunguliwa kwa masoko hayo kunatokana na agizo la Rais John Magufuli la kutaka kila mkoa ambako kuna shughuli za uchimbaji wa madini kufungua soko ili kuwarahisishia wachimbaji wadogo kuuza madini yao, lakini pia kudhibiti tatizo la utoroshaji wa madini uliokuwa ukifanywa hapo awali.

Soko la kwanza kufunguliwa lilikuwa Soko Kuu la Dhahabu mkoani Geita ambalo lilifunguliwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Machi 17, mwaka huu.

Akizungumza , Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, alisema mpaka ilipofika Mei 30, mwaka huu, jumla ya masoko 26 ya madini yalikuwa yameshafunguliwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Aliyataja masoko hayo kuwa ni pamoja na soko la madini la Geita, Kahama, Singida, Chunya, Ruvuma, Shinyanga, Katavi, Dodoma, Kigoma, Tabora, Mara, Mbeya, Kagera, Iringa, Mwanza, Songwe, Tanga, Mbulu-Manyara, Babati-Manyara, Kilimanjaro, Morogoro, Handeni, Lindi, Simiyu na Rukwa.

Profesa Msanjila alisema idadi hiyo inaweza kuwa imeongezeka hadi kufikia masoko 30 mpaka sasa kwa kuwa yanaendelea kufunguliwa, likiwemo soko la madini ya vito ambalo lilifunguliwa jana wilayani Ulanga mkoani Morogoro.

Kuhusu ufanisi wa masoko hayo, alisema hadi Mei 31, mwaka huu, jumla ya Sh bilioni 3.85 zilikuwa zimekusanywa kutokana na mrahaba, Sh milioni 64.25 kutokana na ada ya ukaguzi na Sh milioni 76.85 kutokana na ushuru wa huduma.

Alisema mafanikio hayo yametokana na wananchi kuelewa umuhimu wa kulipa kodi, serikali kuweka mazingira mazuri ya ulipaji wa kodi hizo pamoja na kuboreshwa kwa utendaji wa kisekta ambapo mchimbaji mdogo analipwa fedha yake hapo hapo.

Akiwa mkoani Mbeya kwa ziara ya kikazi, Rais Magufuli alitoa siku saba kwa wakuu wa mikoa wote ambao kwenye mikoa yao kuna shughuli za uchimbaji wa madini kuhakikisha wanafungua masoko hayo.
Mpya zaidi Nzee zaidi