CWT kuendelea kushughulikia kero mbalimbali za walimu


Na Mwandishi wetu Tuduma

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) Komredi Mwalimu Deus G. Seif amewahakikishia walimu nchini kuwa CWT iko pamoja nao katika kutatua matatizo  na kero mbalimbali zinazowakabili hasa suala la upandishwaji wa madaraja,ulipwaji wa madeni yasiyo ya mishahara, nyongeza za mishahara na uwajibikaji wa CWT kwa wanachama wake.

Ameyasema hayo leo mjini Tunduma wakati akiongea na walimu wa Halmashauri hiyo waliojitokeza kwa wingi kumsikiliza na kuelezea kero mbalimbali ambazo wamekua wakikumbana nazo katika kutimiza majukumu yao ya kila siku.

“CWT tumekutana na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Mheshimiwa Waziri Mkuu, Waziri wa Tamisemi,Waziri wa Utumishi pamoja na viongozi wengine  mbalimbali na tumekubaliana kuyafanyia kazi masuala yote ambayo yanawakabili walimu na  kwa kuanzia tayari serikali imetoa barua ya upandishwaji wa madaraja kwa walimu nchi nzima waliokuwa kwenye bajeti  kulingana na kila Halmashauri ilivyokua imejiwekea na tayari walimu wetu wengi wameanza kupata mishahara mipya kutokana na madaraja mapya.” Amesema Katibu Mkuu mwalimu Seif.

Sambamba na hilo amewahakikishia walimu kuwa mali zao ziko salama na hakusita kutolea mfano benki ya Mwalimu(MCBL) na kampuni tanzu ya walimu (TDCL) ambazo mpaka sasa uendeshaji wake unaeleweka na upo katika mstari uliyonyooka, aidha ametumia fursa hiyo kuwakumbusha wanahisa wote nchini wa benki ya mwalimu kuhakikisha wanahudhuria mkutano mkuu wa mwaka wa benki hiyo utakaofanyika tarehe 22 Agosti 2019 Mkoani Mtwara.

Kuhusu suala la hisa za wanachama Seif amesema  ziko salama na benki yao inaendelea kukua na mpaka sasa wanaendelea na mazungumzo na moja kati ya benki iliyoenea nchini na baada ya  makubaliano huduma za Mwalimu Commercial bank zitapatikana nchi nzima kupitia matawi ya benki hiyo watakayokubaliana.

kwa upande wa Mweka hazina wa chama Mwalimu Abubakar Allawi amewahakikishia walimu nchini kupitia mkutano huo kuwa rasimali fedha zote za chama ziko salama na fedha zote za chama zinatoka kwa miongozo, taratibu na kanuni za chama hakuna kiongozi anayefaidika na fedha za wanachama.

Katika mkutano huo Chama Cha Walimu Tanzania(CWT) kupitia kwa Katibu Mkuu wametoa mifuko mia mbili (200) ya saruji  kwa ajili ya ujenzi wa vyoo vya walimu wilayani Momba.