https://monetag.com/?ref_id=TTIb Dkt. Bashiru apiga marufuku wajumbe wa mashina kukaa foleni ofisi za Serikali | Muungwana BLOG

Dkt. Bashiru apiga marufuku wajumbe wa mashina kukaa foleni ofisi za Serikali


Katika muendelezo wa ziara yake Mkoani Mwanza,  Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Bashiru Ally amefika wilayani Magu, ambapo katika vikao vitatu tofauti amesisitiza mabalozi nchi nzima kutokupanga foleni katika ofisi yeyote ya Serikali ama ya CCM.

Akiambatana na viongozi wa chama na serikali wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mwanza Ndg. Anthony Diallo, Katibu Mkuu amekutana na wanachama, mabalozi, na wajumbe wa halmashauri kuu za kata zote na matawi yote wilayani Magu katika vikao vitatu tofauti.

Katibu Mkuu ameeleza kuwa, mabalozi nchi nzima hawatakiwi kukaa foleni katika ofisi yoyote ya serikali na chama, kuanzia ofisi za watendaji wa mitaa, watendaji wa kata, wakuu wilaya, wakurugenzi, wakuu wa mikoa mpaka ofisi za wizara yoyote nchini, kwa sababu mabalozi ndio watu wanaofanya kazi kuliko kiongozi yeyote, kwa kuhangaika na changamoto za mwananchi mmoja mmoja katika eneo lake, bila ya mshahara na wanajitolea wakati wote.

“Nitoe rai kwa niaba ya Chama Cha Mapinduzi nchi nzima kwa viongozi wa serikali na Chama, wakuu wilaya na mikoa, wakurugenzi wote wa Halmashauri nchi nzima, makatibu wa wilaya na mikoa nchi nzima, hawa viongozi wetu wajumbe wa mashina ni marufuku kukaa foleni kwenye ofisi zenu, hawa ni viongozi na wamebeba watu nyuma yao, wanapokuja ofisini wanakuja kueleza hisia, changamoto na ushauri wa watu wao wanaowaongoza. Kiongozi yeyote atakaye wadharau mabalozi wetu huyo hatufai ndani ya Chama na serikali hii ya CCM.” Dk. Bashiru amesisitiza.

“Wajumbe wa mashina ni watu muhimu sana na wamekuwa wakifanya kazi hizi ngumu kwa uzalendo wao pasipo malipo ya mshahara, wanajitoa wakati wote kusaidia watu, wanajua changamoto za mwananchi mmoja mmoja na wakati mwingine hawalali kwa ajili ya shida za watu wanaowaongoza, wanafanya yote haya kwa kujitolea na uzalendo kwa nchi yetu, sitaki nisikie wanawekwa foleni katika ofisi yoyote ya umma, hata ofisini kwangu nikisikia balozi amekuja kutaka kuongea na mimi ni lazima nimpe kipaumbele kwa sababu najua hawa ndio wanaishi na watu,” Dkt. Bashiru amefafanua.

Katika vikao hivyo, Dk. Bashiru amepata fursa ya kusikiliza kero za wananchi, ambapo wananchi wameonesha kuwa na hamu kubwa ya kusikilizwa kero zao za muda mrefu na kutopata wasaa wa kukutana na viongozo wa maeneo yao, kuelezwa na kufafanuliwa mambo mbalimbali yanayohusi changamoto zao.