Baada ya klabu ya Inter Milan ya Italia chini ya kocha wake Antonio Conte kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Manchester United, Romelu Lukaku wamekubali kuwapa Bayern Munich, Ivan Perisic kwa mkopo wa mwaka mmoja.
Perisic alionekana kuwa na maisha magumu ndani ya Inter tangu Mei 31 ya mwaka huu Conte alipoanza kuifundisha timu hiyo kutokana na mfumo.
Wawili hao hawakuweza kuwa na maelewano mazuri tangu Conte alipomtaka Perisic kucheza kama beki wa kupanda na kushuka jambo ambalo hakupendezwa nalo.
Hata hivyo Bayern wamekubali kumchukua Perisic kwa makubaliano ya kuuziwa mchezaji huyo kwa ada ya paundi milioni 30 hapo baadae.
