Bondia machachari nchini, Hassan Mwakinyo ameiomba Serikali isapoti mchezo wa ngumi ili utumike katika kulitangaza taifa nje ya mipaka yake.
Mwakinyo ambaye ni balozi wa Kampuni ya Sportpesa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari juu ya mwelekeo wa ngumi za kulipwa nchini.
Nyota huyo amesema kuwa mabondia wengi wamekuwa na nia ya kulitangaza taifa nje ya mipaka yake kwa kuhakikisha wanashinda mapambano lakini sapoti ya serikali imekuwa ni ndogo ukilinganisha na ile inayoenda kwenye michezo mingine.
"Kazi yetu ni kubwa na ngumu, Serikali imekuwa ikitupa sapoti lakini bado haitoshi isipokuwa tunaomba izidi kutusaidia kwani bado safari ni ndefu."
"Tunaona jinsi wanavyoipa sapoti timu ya taifa ya mpira wa miguu, sasa na sisi tunahitaji sapoti ya namna hiyo ili tuzidi kuipeperusha vyema bendera yetu," amesema Mwakinyo.
Ameongeza kuwa anaamini kuwa serikali ni sikivu na itaunga mkono timu. Mwakinyo anatarajia kupanda ulingoni Oktoba 26 na inaelezwa kuwa huenda atavaana na bondia kutoka Argentina, Ufilipino, Italia, Marekani au Urusi.
