Rais wa Bolivia Evo Morales ajiuzulu

Rais wa Bolivia Evo Morales ameamua kuachia ngazi kwenye uongozi wa nchi, baada ya wiki tatu za maandamano makubwa dhidi ya kuchaguliwa kwake tena kwa muhula wa nne. Hatua hiyo imekuja wakati jeshi na polisi walikuwa wamemtaka aondoke madarakani.

Baada ya wiki tatu za maandamano makubwa na kupoteza imani kwa jeshi, Hatimaye Evo Morales ameaamua kujiuzulu kwenye wadhifa wake wa urais wa Bolivia.

"Ninaachia nafasi yangu kama rais," kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 60, ambaye amekuwa madarakani tangu 2006, amesema kwenye runinga ya taifa Jumapili Novemba 10.

"Jaribio la mapinduzi limefanyika," ameongeza Makamu wa rais Alvaro Garcia Linera, ambaye pia amejiuzulu.

"Tumezindua somo kwa ulimwengu, kesho Bolivia itakuwa nchi mpya," amebaini rais wa zamani Carlos Mesa, kiongozi wa upinzaji na mgombea aliyeshindwa katika uchaguzi wa urais wa Oktoba 20, wakati maelfu ya wananchi wa Bolivia walikuwa wakisherehekea mitaani hatua hiyo ya kujiuzulu kwa rais Evo Morales na makamu wake Alvaro Garcia Linera.

Raia walikuwa wakipinga serikali waliingia mitaani na kusherehekea ushindi wao.

Saa moja kabla ya hatu hiyo ya kujiuzulu, Mkuu wa majeshi ya Bolivia alikuwa amemtaka rais Evo Morales kung'atuka madarakani.

"Baada ya kutathmini hali ya mzozo wa ndani unaoendelea, tunamwomba rais ang'atuke madarakani ili amani na usalama viweze kutawala, kwa faida ya Bolivia yetu," Jenerali Williams Kaliman aliwaambia waandishi wa habari.