Watumishi wahaha kusaka Nyumba usiku na mchana, kisa?


Na. Hamisi  Abdulrahmani, Masasi

Watumishi wa Halmashauri ya wilaya ya Masasi Mkoani Mtwara wanaendelea kuhaha usiku na mchana kutafuta nyumba za kupanga katika kijiji cha Mbuyuni baada ya nyumba za wananchi wa kijiji hicho kuwa chache lakini pia kupandishwa kodi ghafla, kufuatia halmashauri hiyo kuhamia rasmi katika kijiji hicho.

Hayo yalisemwa jana na mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo,Changwa Mkwanzu alipokuwa akitoa taarifa fupi kwa Mkuu wa Mkoa wa Mtwara,Gelasius Byakanwa kuhusu utekelezaji wa agizo la raisi, Dk.John Magufuli la kuhamia kwenye eneo lake la utawala katika kijiji cha Mbuyuni

Mkwanzu alisema moja ya changamoto wanayokutanayo watumishi tangu ofisi za Halmashauri zilipohama mjini na kuhamia kwenye eneo lake la utawala katika cha Mbuyuni watumishi kukosa nyumba za kupanda.

Alisema kuna uhaba wa nyumba za kupangisha katika kijiji hicho ambapo kwa sasa ndio makao makuu ya ofisi za Halmashauri na hata zile zinazopangishwa kodi imepandishwa.

Mkwanzu alisema kodi ya nyumba kwa mwezi imepanda kwa baadhi ya nyumba kijijini hapo kutoka sh.10,000 hadi kufikia kati ya sh.20,000 hadi 30,000 kwa sasa.

 Alisema hali hiyo inasababisha baadhi ya watumishi wawe na ratiba ya kila siku kupanda magari ya abiria kutoka mjini hadi Mbuyuni ziliko ofisi za muda kwa sasa.

Alieleza kuwa watumishi hao ulazimika kila asubuhi kupanda magari ya abiria kwenda ofisini na baada ya muda wa kazi kumalizika kurudi mjini kwa vile hawajapata nyumba za kupanga hadi sasa kijijini hapo.

Mkwanzu alisema kutokana na adha hiyo kwa watumishi hao baadhi ya kazi wanashindwa kuwahumia wananchi ipasavyo.

"Tunataka kila mtumishi hakae huku huku kijijini Mbuyuni tulikohamia lakini changamoto kubwa hapa nyumba za kupanga watumishi hakuna lakini zimepangishwa kodi baada tu ya kuhamia huku ofisi zetu, " alisema Mkwanzu

 Alisema tatizo lingine ambalo limekuwa changamoto baada ya kuhamia kwenye eneo lake la utawala kwenye majengo ya hospitali ya wilaya ni ukosefu wa huduma ya umeme.

Mkwanzu alisema zipo bàadhi ya kazi ambazo zinahitaji umeme na katika majengo hayo waliopo hakuna huduma hiyo hivyo kulazimika kurudi mjini kufuata umeme.

Mmoja wa mtumishi wa Halmashauri hiyo ambaye hakutaka kutaja jina lake gazetini alisema wanalazimika kutumia kati ya sh.5000 hadi sh.6000 kwenda na kurudi ofisini kwa vile hawana nyumba za kuishi.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa aliwapongeza watumishi hao kwa kutekeleza agizo hilo la raisi la kutaka wahamie kwenye eneo lao la utawala.

Byakanwa alisema watumishi wanapaswa kuwa na fikra za kutumia fursa hiyo kuwekeza shughuli za kiuchumi ndani ya kijiji hicho ili kujitelea maendeleo.

Aidha, Mkuu wa Mkoa huyo aliitaka Halmashauri hiyo kutumia majengo waliyoyahama mjini kama kitega uchumi cha mapato kwao.