Umoja wa Ulaya waitaka Iran idumishe mkataba wa nyuklia

Mkuu wa sera za mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya Josep Borrel ameitaka Iran iendelee kuutekeleza mkataba wa nyuklia.

Bwana Borrel alitoa wito huo alipokutana na waziri wa mambo ya nje wa Iran Mohammed Javad Zarif mjini New Delhi.

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya amesisitiza kwa waziri Zarif kwamba mkataba huo sasa ni muhimu zaidi kutokana na kuongezeka kwa mivutano katika Mashariki ya Kati.

Wanadiplomasia hao wawili walifanya mazungumzo ambapo bwana Borrel alisisitiza azma ya Umoja wa Ulaya ya kuudumisha mkataba wa nyuklia.

Mkataba huo ulifikiwa kati ya Iran na mataifa makubwa duniani mnamo mwaka 2015 lakini ulianza kutetereka baada ya Marekani kuamua kujiondoa takriban miaka miwili iliyopita.

Na mapema wiki hii Ujerumani,Ufaransa na Uingereza zilianzisha mchakato wa kuwezesha kurejeshwa kwa vikwazo vya Umoja wa Mataifa dhidi ya Iran baada ya nchi hiyo kutangaza kuendelea kurutubisha madini ya Urani kuvuka kiwango kinachoruhusiwa.

Waziri wa mambo ya nje wa Iran bwana Zarif amezilaumu nchi za Ulaya kwa kufanya usaliti.