DC Kitundu awataka wazazi kuandaa watoto wao wa kidato cha Sita kurejea Shuleni Juni Mosi



Na John Walter-Babati

Baada ya serikali kuruhusu Vyuo na kidato cha sita kuendelea na masomo, Mkuu wa wilaya ya Babati, Elizabeth Kitundu amesema kuwa Maafisa elimu wapo katika mikakati ya kuweza kuwataarifu rasmi wakuu wa shule zenye kidato cha sita ili wanafunzi waandaliwe kurejea shuleni juni mosi.

Amesema mpango huo unahusisha shule za Serikali na binafsi kama lilivyo agizo la waziri wa Elimu.

Kitundu amesema kuanzia leo atawaandikia barua rasmi wakuu wa shule kuhusu hatua hiyo ya serikali mara baada ya kuwa nyumbani kwa zaidi ya miezi miwili sasa baada ya ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID19) kuingia hapa nchini Machi 16 mwaka huu. 

Amewataka wazazi na walezi wawaandalie mahitaji yote muhimu watoto wao ili kurejea shuleni na kwa ajili ya maandalizi ya mitihani ya kuhitimu kidato cha sita.

Hatua hiyo ya kufunguliwa kwa shule za sekondari kwa wanafunzi wa  kidato cha sita na vyuo ilitangazwa na Rais John Pombe Magufuli  wakati alipokuwa akiwaapisha viongozi aliowateua hivi karibuni.

Rais Magufuli alisema vyuo vikuu vyote sasa vitarejea katika hali yake ya kawaida kuendelea na masomo kuanzia Juni Mosi baada ya kijiridhisha kutokana na maendeleo ya hali ya maambukizi ya virusi vya corona.
Mpya zaidi Nzee zaidi