Mkurabita yatoa hati za hakimiliki za kimila 856 wilayani Sikonge


JUMLA ya Hati za Hakimiliki za Kimila 856 zimetolewa kwa Wanakijiji wa Vijiji vitatu vya Wilaya ya Sikonge baada ya maeneo yao kuhakikiwa na kupimwa chini ya Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA)

Kauli hiyo imetolewa leo na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya  Wilaya ya Sikonge Tito Luchagula wakati akisoma taarifa ya mpango wa matumizi bora ya ardhi katika sherehe fupi za kukabidhi hati za Hakimiliki za Kimila kwa vijiji vya  Ukondamoyo, Mole na Usanganya.

Alisema kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi chini ya uratibu wa MKURABITA ulianza  kutekelezwa katika vijiji hivyo kuanzia mwaka wa fedha wa 2009/10 ambapo awamu ya kwanza walitoa hati za hakimiliki za kimila 632  na awamu ya pili wameandaa hati 224 na kufikisha 856.

Luchangula alisema katika sehemu ambazo MKURABITA umetekelezwa umesaidia kuwa na matumizi bora ya ardhi na kuondoa migogoro ya ardhi baina ya mwananchi mmoja na mwingine.

Meneja wa Urasimishaji Ardhi wa Mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (MKURABITA) Antony Temu alisema hadi hivi sasa wamefikisha huduma hiyo katika Halmashauri 52 kwa upande wa Tanzania bara.

Aliwataka Wanavijiji walionufaika kwa kutambuliwa na kupimiwa maeneo yao na kupata Hati za Hakimiliki za Kimila kuzitumia katika kuboresha kilimo na mitaji yao kwa ajili ya maeneo ya familia zao na Taifa kwa ujumla.

Temu alisema hizo zitawasaidia kuunganishwa na Taasisi za fedha ambazo zitawawezesha kupata mitaji ya kuendesha kilimo na ufugaji wa kibiashara ambao utainua uchumi wao.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi