RC Mghwira awaundia mkakati walimu wanaocharaza wanafunzi viboko bila utaratibu

 


Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira amesema Serikali itachukua hatua kali dhidi ya shule zitakazobainika kuwacharaza viboko wanafunzi kwa lengo la kuwafanya wawe na nidhamu.


Amesema ana taarifa baadhi ya shule wanafunzi wanachapwa viboko na kupata majeraha mwilini jambo alilodai kuhatarisha usalama wao.


Ameeleza hayo leo Jumatano Januari 13, 2021 katika mkutano wake na waandishi wa habari, akibainisha kuwa viboko huwafanya wanafunzi kuchukia shule kwa kuwa wanaona wananyimwa uhuru wa kujifunza.


“Ninapenda kutoa angalizo kwa shule zote zenye walimu wanaotumia adhabu ya viboko kama sehemu ya kufundishia nidhamu shuleni. Na hii imethibitika kisayansi kuwa kadiri mwalimu anavyotumia viboko ndivyo anavyopunguza uwezo wa mwanafunzi kujifunza na kuelewa,” amesema mkuu huyo wa Mkoa.


Katika maelezo yake amesema, “kama ni adhabu lazima kuzingatia usalama wa mwanafunzi na afya ya akili ili kuzuia hali ya mwanafunzi kumwogopa mwalimu kupita kiasi ama kuchukia masomo na kusababisha utoro.”


“Tuna taarifa za shule ambazo zinapiga wanafunzi, unakuta mwanafunzi ana alama mgongoni, miguuni, amechanwa ngozi ,ametoka sugu mkononi kwa ajili ya kuchapwa. Wengine wanachapwa hadi kukimbia shule, nimeletewa malalamiko na baadhi ya wazazi na mimi nilienda kwenye hiyo shule kuthibitisha nikakuta ni kweli.”


Amesema hali hiyo imesababisha wanafunzi waliokuwa wanafanya vizuri katika masomo yao kuanza kufanya vibaya na kutaka walimu kuwafanya wanafunzi kuwa marafiki ili wasiwaogope.


“Najua sheria imeainisha aina za adhabu zinazoweza kutolewa kwa wanafunzi..., tukiwabaini walimu sheria itafuata mkondo wake kama kawaida,” amesema Mghwira

Post a Comment

0 Comments