JKT yawaita kambini vijana wa kujitolea kuanza mafunzo rasmi


Na Ezekiel Mtonyole - Dodoma.

Mkuu wa Jeshi la kujenga taifa JKT Meja Jenerali Charles Mbuge amewaarifu vijana wa kujitolea waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya JKT  kwa mwaka 2020/2021 kuripoti makambini ambao awali walirejeshwa majumbani.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Chamwino Mkoani Dodoma Kaimu Mkuu wa utawala JKT Kanali Hassani Mabena amesema vijana wanaotakiwa kuripoti kambini ni vijana wa darasa la saba na kidato cha nne wakati makundi mengine yakisubiri taarifa nyingine.

"Mkuu wa Jeshi la kujenga taifa (JKT) Meja Jenerali Charles Mbuge anautaarifu Umma kuripoti makambini vijana waliochaguliwa kujiunga na mafunzo ya JKT kwa kujitolea kwa mwaka 2020/2021 ambao mwezi februari 2021 walirejeshwa majumbani" amesema Kanali Mabena.

Amesema watakaorejea kambini ni wale tu ambao awali walipangiwa katika makambi mbalimbali na sasa watatakiwa kurejea kwenye kambi zao za awali ni wale wenye elimu ya darasa la saba na kidato cha nne ambao wanatakiwa kuanza kuripoti kuanzia Mei 7 hadi Mei 14, 2021.

"Vijana wanaotakiwa kuripoti makambi ya JKT waliyopangiwa hapo awali ni wale wenye elimu ya darasa la saba na elimu ya kidato cha nne waripoti makambini kuanzia tarehe 7 Mei hadi tarehe 14 Mei 2021" amesema.

Aidha Kanali Mabena amesema kwa vijana wenye elimu ya kidato cha sita, na wenye elimu ngazi ya cheti, Stashahada, Shahada, na wale wenye taaluma ya uhandisi wataendelea kusubiri majumbani hadi hapo utaratibu mwingine utakapo kamilika na utatangazwa.

 

Post a Comment

0 Comments