Na Amiri Kilagalila,Njombe
Mwenyekiti
wa umoja wa wanawake wa Chama cha Mapinduzi (UWT) mkoa wa Njombe
Scolastika Kevela amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uteuzi wa
mawaziri wapya watatu wakiwemo wanawake wawili hatua aliyodai imeendelea
kuleta uwiano wa kijinsia katika uongozi nchini.
Akizungumza
na vyombo vya habari Mwenyekiti huyo ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji
wa Kampuni ya Udalali ya Yono Auction Mart alisema uteuzi wa Waziri wa
Ulinzi Dkt. Stergomena Tax pamoja na Waziri wa Habari,Mawasiliano na
Teknolojia ya Habari, Dkt. Ashatu Kachwamba Kijaji kimeonyesha nia njema
ya Rais Samia kuwaheshimisha wanawake.
Mbali
na Mawaziri hao Rais Samia pia alimteua Mbunge wa Bumbuli January
Makamba kuwa Waziri wa Nishati na Madini akichukua nafasi ya Dk Medard
Kalemani ambaye uteuzi wake pamoja aliyekuwa Waziri Habari,Mawasiliano
na Teknolojia ya Habari Dk Faustine Ndugulile na aliyekuwa Waziri wa
Uchukuzi Dk Leonard Chamriho, ulitenguliwa.
"Kwa
niaba ya wanawake wote wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Njombe
tunampongeza Rais Samia kwa uteuzi huu, na zaidi tunatambua jitihada
zake za kuhakikisha wanawake wanashika nafasi muhimu kwa mustakabali wa
nchi yetu,nafasi ambazo kwa muda mrefu zimekuwa zikishikiliwa na
wanaume"alisema Scolastika
Amesema
uteuzi huo umeifanya Tanzania kutengeneza historia kwa kuwa na Waziri
wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa ambaye ni mwanamke lakini pia
mwanamke wa kwanza kuwa waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari
Kimsingi uteuzi
huo umeongeza nafasi za wanawake mawaziri kufikia 7 sawa na asilimia
30.4 kutoka 5 sawa na asilimia 21.7 huku wanaume wakiwa ni 16 sawa na
asilimia 69.6 jambo alilosema ni mwelekeo mzuri katika kufikia idadi ya
hamsini kwa hamsini.
"Nitoe
wito kwa viongozi wanawake na wanaume waliopo katika nafasi mbalimbali
za uteuzi kutumia nafasi zao kikamilifu na kumsaidia Rais ili aweze
kutimiza vyema majukumu yake ya kuleta maendeleo endelevu na jumuishi
kwa Taifa letu" aliongeza Scolastika
