Vifo vya watu 27 vilivyotokea jana katika mlango wa bahari wa kuingilia Uingereza vinaendelea kuzidisha mvutano kati ya Uingereza na Ufaransa juu ya namna ya kuwazuwiya wahamiaji kuvuka kuingia Uingereza kutumia maboti madogo.
Licha ya ahadi kutolewa na waziri mkuu Boris Johnson na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kwamba watafanya kila wawezalo kuzuwiya biashara haramu ya kuwasafirisha watu inayogharimu maisha ya wahamiaji, wanasiasa wa pande zote mbili tayari wameanza kulaumiana kushindwa kuzuwiya mkasa uliotokea jana Jumatano.
Maafisa wa Uingereza wameikosoa Ufaransa, kukataa pendekezo lao la polisi wa Uingereza na maafisa wa mpakani kushirikiana kulinda eneo la pwani , huku Ufaransa ikisema Uingereza inachochea mzozo maana ni rahisi kwa wahamiaji kubakia nchini humo na kufanya kazi iwapo watafanikiwa kuvuka mlango wa bahari na kuingia Uingereza.
Uingereza kupitia waziri wake wa mambo ya ndani Priti Patel imesema inaendelea kuzungumza na mataifa mengine kutafuta suluhu naye rais wa Ufaransa Emmanuel Macron anatarajiwa kuzungumzia suala hili na maafisa wengine wa Ulaya.