Marekani na baadhi ya washirika wake muhimu wamepongeza kura ya maoni ya mabadiliko ya katiba iliyopangwa kufanyika Serbia Januari 16.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani leo imetoa taarifa ya pamoja na Ufaransa, Ujerumani, Italia, Uingereza, Marekani na Umoja wa Ulaya ambayo inaelezea kura hiyo kama hatua muhimu kuimarisha uhuru wa mahakama.
Nchi hizo zimesema zinatambua kwa masikitiko kwamba serikali ya Kosovo haijaliruhusu Shirika la Usalama na Ushirikiano barani Ulaya OSCE kukusanya kura za wapiga kura wanaoishi Kosovo.
Taarifa hiyo imeitaka Kosovo kuwaruhusu Waserbia walioko nchini humo kutekeleza haki yao ya kupiga kura. Mwaka uliopita, wabunge wa Serbia waliidhinisha Januari 16, kuwa siku ya kupiga kura ya maoni ya marekebisho ya katiba ambayo yataondoa ushawishi wa kisiasa katika uteuzi wa waendesha mashtaka na majaji ili kuisadia Serbia kukidhi vigezo vya kujiunga na Umoja wa Ulaya.