Wananchi Ruangwa waeleza Tasaf ilivyobadilisha maisha yao


Baadhi ya wakazi wa wilaya Ruangwa mkoani Lindi wamesema kupitia Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (Tasaf) wamenufaika kwa kuanzisha biashara za ufugaji wa kuku na mbuzi.


Hayo yameelezwa leo Januari 14 na baadhi ya wanufaika hao walipozungumza na Mwananchi.


Miongoni mwa wanufaika nao ni Fatuma Chikopa ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Namkonjera wilayani  Ruangwa aliyesema alipokea Sh34,000 ambazo zimemsaidia kuanzisha mradi wa ufugaji wa kuku na huduma kwa watoto  wawili na wajukuu zake watatu.


 "Baada ya kupata fedha za Tasaf niliamua kuwekeza katika mradi wa ufugaji kuku nilianza na wawili Sasa Nina Hamsini," amesema Fatuma


Naye mkazi wa Kijiji cha Likangala, Zainabu Makolela amesema kuwa amekuwa akipokea Sh24,000 kila baada ya miezi miwili ambazo zimekuwa sikimsaidia kupata mtaji wa kununua kuku.


Zainabu amesema anapokea fedha hizo kwa awamu nane na zimemsaidia kuanzusha mradi wa kufuga kuku, hivyo amejiongezea kipato na anatarajia kuwekeza zaidi  katika ufugaji wa mbuzi, kondoo na baada ya kuuza  kuku na bata ili kujiongezea kipato na kuondokana na umaskini.


Kwa upande wake Musa Kumkana wa kijiji hicho, amesema kuwa maisha yake yamebadilika, baada ya kuingizwa kwenye mpango wa Tasaf wa kaya masikini ambapo anapokea Sh50,000 zilizomsaidia kuanzisha mradi wa ufugaji wa bata na Mbuzi ambao wanaendesha maisha yake.


Akizungumzia mradi huo, mratibu wa Tasaf wilayani Ruangwa amesema mpango ulianza mwaka 2014 ikiwa na kaya 5,143  kwenye vijiji 52 Kati 90 vya  wilaya hiyo, lakini baadaye waliongeza kujitambua  vijiji 38 ambayo vitaingia kwenye mpango mpya  na kuwa na jumla kaya 8,183 ambayo vitanufaika na mpango huyo.


 Chibanda amewataka wanufaika hao kutumia fursa hiyo ya Tasaf ili kujiinua kiuchumi kwani ikiondoka wawe na miradi endelevu waendelee kufanya  shughuli zao bila kuhitaji msaada.

Chapisha Maoni

Mpya zaidi Nzee zaidi