Ticker

6/recent/ticker-posts

 


Tetemeko la ardhi Afghanistan:Taliban yaomba msaada wa kimataifa

 


Kundi la Taliban nchini Afghanistan limeomba msaada wa kimataifa, huku nchi hiyo ikikabiliana na athari za tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 6.1 katika kipimo cha Richter.


Zaidi ya watu 1,000 wameuawa na takriban 1,500 wamejeruhiwa. Idadi isiojulikanaya watu imezikwa kwenye vifusi vya nyumba zilizoharibiwa, mara nyingi zilizojengwa kwa udongo.


Mkoa wa Kusini-mashariki wa Paktika umeathirika zaidi na Umoja wa Mataifa unahangaika kutoa makazi ya dharura na msaada wa chakula.


Juhudi za uokoaji zinatatizwa na mvua kubwa na ukosefu wa rasilimali.


Manusura na waokoaji wameiambia BBC kuhusu vijiji vilivyoharibiwa kabisa karibu na kitovu cha tetemeko hilo, barabara zilizoharibika na minara ya simu za rununu - na hofu yao kwamba idadi ya vifo itaongezeka zaidi.


Tetemeko hilo ni baya zaidi kuwahi kuikumba nchi hiyo katika miongo miwili ni changamoto kubwa kwa kundi la Taliban, vuguvugu la Kiislamu ambalo lilipata mamlaka tena mwaka jana baada ya serikali inayoungwa mkono na nchi za Magharibi kuanguka.


Tetemeko hilo la ardhi lilipiga takriban kilomita 44 kutoka mji wa Khost na mitetemeko ilisikika katika maeneo ya mbali kama Pakistan na India.


Afghanistan iko katikati ya mzozo wa kibinadamu na kiuchumi, na Abdul Qahar Balkhi, afisa mkuu wa Taliban, alisema serikali "haina uwezo wa kifedha kusaidia watu kwa kiwango kinachohitajika".


Mashirika ya misaada, nchi jirani na mataifa yenye nguvu duniani yalikuwa yanasaidia, alisema, lakini akaongeza: "Msaada huo unahitaji kuongezwa kwa kiwango kikubwa sana kwa sababu hili ni tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijapata kutokea kwa miongo kadhaa."


Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres alisema shirika hilo "limejipanga kikamilifu" kuhusu maafa hayo. Timu za afya, vifaa vya matibabu, chakula, na makazi ya dharura vilikuwa njiani kuelekea eneo la tetemeko hilo, maafisa wa Umoja wa Mataifa walisema.

Post a Comment

0 Comments