Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Dkt.Francis Michael ameutaka Uongozi wa Mamlaka ya Ufundi Stadi nchini (VETA) kujiandaa na mageuzi ya elimu ili kuhakikisha wahitimu wanaozalishwa na vyuo vilivyopo chini ya Mamlaka hiyo wanaajirika na kujiajiri.
Akizungumza na
Uongozi pamoja na Watumishi wa VETA Makao Makuu jijini Dodoma, Dkt. Michael
amesema dhamira ya Serikali ni kuwa na elimu itakayosaidia wahitimu kufikiria
fursa zilizopo na kuzitumia ili kutengeneza maisha yao na kuchangia katika
uchumi wa Taifa.
“Tunatakiwa
tuzalishe wahitimu ambao wanafikiri na kuwa na uwezo wa kujitengenezea kipato
kutokana na fursa zinazowazunguka, tumeamua kwenda kwenye elimu ujuzi
(competence based) hivyo VETA lazima mjiandae ikiwemo kuanzisha kozi hadi za
Kilimo.” amesema Dkt. Michael.
Katika ziara hiyo,
Dkt. Michael pia alisikiliza na kutoa ufafanuzi juu ya changamoto mbalimbali
kutoka kwa watumishi wa mamlaka hiyo.
Sanjari na hayo, Dkt. Michael ametembelea na kukagua kiwanda cha utengenezaji wa samani kinachomilikiwa na Mamlaka hiyo kilichopo jijini Dodoma.

