Na Ezekiel Mtonyole – Dodoma.
Serikali kwa kushirikiana na Shirika Umoja wa Mataifa la
Chakula Duniani (FAO) na Umoja wa Ulaya (EU) imezindua mradi wa kuimarisha
huduma za Afya ya Mimea na usalama wa Chakula hapa nchini mradi wenye lengo la
kuhakikisha usalama wa Chakula na kuimarisha mfumo wa ukaguzi wa utoaji wa
usafi wa Mazao yanayoingia na kutoka hapa nchini.
Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi huo Naibu Waziri
wa Kilimo Mhe. Antony Mavunde amesema mradi huo utasaidia katika kudhibiti
visumbufu vigeni kwa kuhakikisha mazao yanayoingia au kutoka hapa nchini
yanakuwa na ubora unaokidhi viwango vya kimataifa.
“Niwashukuru EU na FAO kwa kufadhili mradi huu muhimu ni
imani yetu kuwa malengo yaliyopangwa yatafikiwa na hivyo kuongeza upatikanaji
wa masoko ya kimataifa na kuchochea uchumi wa taifa na mtu mmoja mmoja” amesema
Mhe. Mavunde.
Naibu Waziri Mavunde amesema mradi huo umetokana na
ukaguzi uliofanyika hapa nchini mwaka 2017 katika mifumo maalumu ya udhibiti wa
mimea na mazao yanayosafirishwa kwenda nchi za jumuiya ya Ulaya na ukaguzi huo
kubaini mapungufu ya afya ya mimea.
Ametaja baadhi ya maeneo yaliyobainika kuwa na mapungufu hadi kupelekea kuanzishwa kwa mradi huo ni maarifa madogo kwa wakaguzi kuhusu matakwa ya usafi wa mazao hayo, kukosekana kwa mfumo kukusanya takwimu za visumbufu vya mimea, kukosekana kwa maabara zenye uwezo wa kufanya uchunguzi muhimu ili kuthibiti cheti cha usafi wa mimea.
“kufuatia kubainika kwa mapungufu hayo na gharama za
kufanya biashara ya mazao kuwa juu serikali ilichukua hatua kwa kuunganisha majukumu
ya TPRI na ya afya ya mimea na viwatilifu TPHPA ambacho kimekuwa ni chombo
kinachotambilika kimataifa” amesema.
Amesema kuja kwa mradi huu utawezesha kufikia malengo ya
kuhakikisha ukuaji wa sekta ya kilimo hapa nchini kwa asilimia 10 na mauzo ya
mazao ya kilimo yanaongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 1.2 za sasa hadi
kufikia Dola bilioni 5 ifikapo mwaka 2030.
Amesema Wizara ya Kilimo itasimamia utaratibu na kuongeza
utekelezaji wa mradi huo na kutaka kamati ya kusimamia mradi huo na kumtaka
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo kuwasimamia wataalamu ili kazi zilizopangwa
kwenye mradi zitekelezeke kwa wakati.
Awali Mwakilishi wa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo
Bw. Obadia Nyagilo amesema mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha mika mitatu
na nusu kwa kiasi cha Euro milioni 10.1 kwa ushirikiano ambapo Jumuiya ya umoja
wa Ulaya itatoa Euro milioni 9.5, FAO itatoa Euro 350’000 na Tanzania itatoa
EURO 250,000.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Afya
ya mimea na Viwatilifu Tanzania TPHPA Dkt.
Efraim Njau amesema sekta ya kilimo ni muhimu sana ambapo imeajiri zaidi ya
asilimia 67 ya watanzania na kuchangia takribani asilimia 29 ya pato la taifa.
Ametaja baadhi ya majukumu yanayofanywa na TPHPA ni
kusimamia na kuratibu tasnia nzima ya viuatilifu, kudhibiti ubora, uagizaji,
usambazaji na kuchagiza matumizi sahihi na usalama wa viuatilifu, kufanya
uchambuzi wa athari ya visumbufu.
Ameongeza kuwa “matokeo tarajiwa ya mradi huo ni
kuziongezea uwezo maabara za mamlaka kujenga, kukarabati na kuweka vifaa katika
maabara za Mamlaka, kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji wa visumbufu na masalia ya
viuatilifu katika mnyroro wa thamani ya uzalishaji wa mazao hususa ni yale
mbogamboga na matunda” amesema Dkt. Njau.
Aidha amesema mradi utakuwa na kamati ambayo itaundwa na itawajibika kukutana na mara mbili kwa mwaka kupitia na kuhakikisha malengo ya mradi yanakwenda kama yalivyopangwa.
Nae Mwakilishi wa Shirika la Chakula Duniani FAO Bi.
Nyebenyi Tipo amesema mradi huo umelenga kuhakikisha usalama wa Chakula hasa
kwa mazao yanayovuka mipaka kwa kuhakikisha yanakuwa na ubora na kuhakikisha
usalama wa chakula na FAO watatoa ushirikiano kuhakikisha mradi huo
unatekelezeka na unaleta tija kwa kukuza sekta ya kilimo na mazao ya hapa nchi
kupata soko nje.


