Ethiopia ni mwenyeji wa kongamano la kila mwaka la Umoja wa Mataifa la intaneti licha ya kukatika kwa intaneti kwa zaidi ya mwaka mmoja katika eneo lililoharibiwa na vita la Tigray.
Zaidi ya wajumbe 2,500 kutoka kote duniani wanahudhuria kongamano hilo, ambalo linaangazia ''kuwaunganisha watu wote na kulinda haki za binadamu''.
Hata hivyo, uamuzi wa Umoja wa Mataifa kuandaa hafla hiyo mjini Addis Ababa umeibua sintofahamu miongoni mwa wanaharakati wa mtandao na haki za binadamu.
Ni kawaida kwa mamlaka ya Ethiopia kuzima mtandao katika maeneo yaliyoathiriwa na migogoro, na hivyo kufanya iwe vigumu kwa familia kuwasiliana.
Hapo awali, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed alitetea kukatika kwa umeme akisema "intaneti sio maji, mtandao sio hewa" na kuzimwa kulilenga kuokoa maisha.
Aliongeza kuwa maamuzi yalifanywa kuokoa maisha wakati wa migogoro.
