Kamanda wa kikosi cha jeshi la Ukraine Anatoly al maarufu "Kupol", ambaye aliliambia gazeti la Marekani la Washington Post kuhusu kushindwa vibaya kwa vikosi vya Ukraine, alishushwa cheo, limeripoti gazeti la Ukraine "Ukrainian Pravda" likimnukuu afisa wa vikosi vya uvamizi wa anga nchini humo.
Taarifa ya mwanajeshi huyo ilichapishwa baada ya kufanya mazungumzo na kundi la waandishi wa habari wa Marekani ambao walichapisha taarifa hiyo tarehe 13 Machi , kuhusiana na hali katika eneo la Bakhmut kufuatia mashambulizi ya Warusi.
Alidai kuwa kushindwa kwa jeshi la Ukraine katika mapigano ya Bakhmutkulipelekea kupungua pakubwa kwa idadi ya wanajeshi wa Ukraine, jambo ambalo awali liliangaliwa kama faida ya Ukraine ikilinganishwa na Urusi. Matokeo yake , baadhi ya maafisa walianza kuhoji utayari wa Ukraine wa kukabiliana na vita siku zijazo.
Miongoni mwa mambo mengine , kamanda hiyo wa Ukraine alisema kuwa takriban wanajeshi 100 kati ya 500 katika kikosi chake waliuawa na wengine 400 wakajeruhiwa katika mashambulio ya Bakhmut.
Mwakilishi rasmi wa kikosi cha anga cha Ukraine, Valentin Shevchenko, katika mahojiano na gazeti la Ukraine -Ukrayinska Pravda, alisema taarifa zilizotolewa na mwanajeshi huyo zilizidi makadirio na sio za kuaminika na akasema kwamba maafisa wanachunguza zaidi kuhusu taarifa alizozitoa.
